Jinsi wafanyikazi wa Wells Fargo walitoroka na milioni 94 za supermarket maarufu -DCI

Washukiwa waliendesha lori hilo kwa siri kutoka kwa afisi ya kampuni hiyo muda mfupi baada ya pesa kupakiwa ndani.

Muhtasari

•DCI wameanzisha msako wa kuwasaka wafanyikazi wa Wells Fargo wanaodaiwa kutoroka na 94 milioni za duka kubwa maarufu.

•Maafisa wa usalama walipata lori tupu ambalo lilikuwa na pesa hizo likiwa limetelekezwa katika eneo la South C.

Washukiwa Anthony Nduiki na Daniel Mungai
Image: TWITTER// DCI

Makachero wa DCI wameanzisha msako mkubwa wa kuwasaka wafanyikazi wawili wa Wells Fargo wanaodaiwa kutoroka na Ksh 94 milioni za duka kubwa maarufu.

Daniel Mungai Mugetha ambaye ni kamanda wa kikosi na Anthony Nduiki Waigumu, dereva, wanaripotiwa kutoweka na kiasi hicho kikubwa cha pesa baada ya kuliacha gari la kampuni lililokuwa limebeba pesa hizo katika eneo la Dafarm eneo la South C, Nairobi.

Maafisa wa DCI wameripoti kuwa washukiwa waliendesha lori hilo kwa siri kutoka kwa afisi ya kampuni hiyo ya ulinzi jijini Nairobi muda mfupi baada ya pesa kupakiwa ndani. Inasemekana waliacha gari la polisi la kusindikiza lililokuwa likisubiri kuruhusiwa kuondoka.

“Bila kujua kwamba lori nambari. KBA 517T walilokuwa wasindikize lilikuwa limeondoka dakika za awali, timu ya wasindikizaji yenye silaha ilikwenda kuuliza kutoka kwa wasimamizi kwa nini upakiaji ulikuwa unachukua muda mrefu sana. Kufikia wakati huo, hakuna lori wala wafanyakazi walioweza kupatikana,” ilisoma ripoti ya DCI.

DCI waliongeza, “Ripoti ya Meneja wa Uchunguzi wa kampuni hiyo ilionyesha kuwa gari hilo aina ya Isuzu Canter lilikuwa likisafirisha pesa kwa benki moja iliyoko mtaa wa Kenyatta Avenue, Nairobi, na lilibeba Sh94 milioni za duka kubwa maarufu nchini.”

Maafisa wa polisi kutoka Lang’ata ambao walihamasishwa kuwatafuta washukiwa hao baadaye walipata lori tupu ambalo lilikuwa na pesa hizo likiwa limetelekezwa katika eneo la South C.

Maafisa wa upelelezi kutoka tawi maalum tangu wakati huo wameanzisha msako mkali wa kuwatafuta washukiwa na kurejesha pesa zilizoibwa.

DCI pia imetoa picha za washukiwa hao wawili na kuwataka umma kushiriki habari  muhimu zitakazosaidia kukamatwa kwao.