(+picha) Majina, sura za wanafunzi 11 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta waliofariki kwenye ajali zafichuliwa

11 hao walikuwa miongoni mwa kundi la wanafunzi na wafanyikazi 58 waliokuwa wakielekea jijini Mombasa.

Muhtasari

•Wanafunzi  wengine 11 zaidi walijeruhiwa vibaya katika tukio hilo la kusikitisha huku 16 wakinusurika na majeraha madogo.

•Haya yanajiri huku taasisi hiyo ya elimu ya juu ikiendelea kuwaomboleza wanafunzi waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea mapema wiki hii.

Lango la Chuo Kikuu cha Kenyatta
Image: MAKTABA

Utambulisho wa wanafunzi kumi na mmoja wa Chuo Kikuu cha Kenyatta waliopoteza maisha katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea kwenye ya barabara ya Nairobi-Mombasa siku ya Jumatatu umefichuliwa.

Wanafunzi hao ni Navile Omondi Opiyo, Beneas Otieno, Hellen Mbula Kisilu, Michael Muteti, Vallary Akinyi Ouma, na Oslo Mwendwa. Wengine ni; Felix Gori Nyaata, Austine Omondi Owino, Rodger Kiprotich Rono, John Mbiriri Mureithi, na Patricia Murugi Mwangi.

11 hao walikuwa miongoni mwa kundi la wanafunzi na wafanyikazi 58 wa Chuo Kikuu cha Kenyatta waliokuwa wakielekea jijini Mombasa kwa ziara ya kimasomo wakati basi walimokuwa wakisafiria liligongana na trela katika eneo la Maungu, Voi, Kaunti ya Taita Taveta.

Wanafunzi  wengine 11 zaidi walijeruhiwa vibaya katika tukio hilo la kusikitisha huku 16 wakinusurika na majeraha madogo.

Haya yanajiri huku taasisi hiyo ya elimu ya juu ikiendelea kuwaomboleza wanafunzi waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea mapema wiki hii.

Huku wanafunzi na wafanyikazi wakijaribu kukubaliana na tukio hilo la kusikitisha, taasisi hiyo imezindua njia mbalimbali ambazo wataonyesha heshima kwa walioaga.

Katika siku tatu zilizopita, wanafunzi na wafanyakazi wamekusanyika pamoja mida ya jioni ili kuwasha mishumaa kama njia ya kuwakumbuka vijana kumi na mmoja ambao maisha yao yalikatizwa na ajali hiyo.

Tukio hilo linafanyika katika Bishop Square na maelfu walijitokeza katika hafla iliyojaa hisia.

Jumatano, wasimamizi walikuwa walitangaza kuwa kengele maalum itapigwa mwendo wa saa saba mchana na dakika ya kimya pia itazingatiwa.

“Saa saba kamili mchana, kengele ya Campanile italia kwa dakika moja kwa siku tatu zijazo kuanzia leo (Jumatano). Tunawaomba wafanyikazi wote na wanafunzi kunyamaza kwa dakika moja kuwakumbuka wanafunzi wetu walioaga," taasisi hiyo ilitangaza.

Masomo katika chuo kikuu hicho pia yamesimamishwa kwa siku tatu ili kuruhusu wanafunzi na wafanyikazi kuomboleza wenzao.

Kusimamishwa kwa masomo kulianza Jumatano hadi Ijumaa wiki hii.

‘Kufuatia mkasa huu mkubwa, Menejimenti ya chuo kikuu imeamua kusimamisha masomo yote kwa siku tatu kuanzia Jumatano tarehe 20 Machi 2024 ili kutuwezesha kuwaomboleza wanafunzi wetu wapendwa,” taarifa ya Jumanne iliyotiwa saini na msaidizi wa naibu chansela Prof. Waceke Wanjohi ilisoma.

Taasisi hiyo ilifichua kuwa ajali hiyo ilihusisha wanafunzi kutoka idara ya usimamizi wa afya na habari katika Shule ya Sayansi ya Afya.

Ilisema pamoja na wanafunzi kumi na mmoja waliopoteza maisha, wengine kumi na moja walijeruhiwa vibaya huku 16 wakipata majeraha madogo.

"Mipango inafanywa kusafirisha miili ya wanafunzi kumi na mmoja (11) hadi Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kando ya Thika Super Highway," taasisi hiyo ilisema.

Prof Waceke pia alifichua kuwa taasisi hiyo imetenga dawati la usaidizi ili kutoa usaidizi  na pia kujibu maswali kuhusu ajali hiyo.