Ukweli: Bango la tangazo la kampeni la Ruto liliondolewa Kisumu

Muhtasari

•Kampuni ya matangazo imesema  hakuna malalamishi yoyote ambayo wamepokea kuhusu kuondolewa kwa bango hilo.

•Meneja wa Jiji la Kisumu Abala Wanga amezitaka kampuni za utangazaji kufuata utaratibu unaostahili wakati wa kuweka mabango.  

Bango la Naibu Rais William Ruto kabla na baada ya kuondolewa Kisumu.
Bango la Naibu Rais William Ruto kabla na baada ya kuondolewa Kisumu.
Image: HISANI

Kampuni ya utangazaji ya Firmbridfe ambayo ilipachika bango la kampeni la Naibu Rais William Ruto kwenye ubao ulio mjini Kisumu imethibitisha kuwa iliondolewa. 

Kampuni hiyo hata hivyo imesema kwamba hakuna malalamishi yoyote ambayo wamepokea kuhusu kuondolewa kwa bango hilo.

Meneja wa utendakazi wa kampuni hiyo Joseph Odindo alisema bango hilo la matangazo ni mali yao. 

Alisema hawana nia ya kulalamika kwa mtu yeyote juu ya kuondolewa kwa bango hilo. "Hiyo ni mali yetu na hatujalalamika kwa mtu yeyote. Hilo ni mabango yetu," Odindo aliambia Star kwenye simu. 

Hata hivyo, alikataa kuzungumzia zaidi nani aliondoa bango hilo akisisitiza hawana malalamiko.

Haya yanajiri huku baadhi ya wafuasi wa Ruto wakimtuhumu mpeperushaji bendera wa Azimio, Raila Odinga, kwa kuondolewa kwa bendera ya kampeni.

 Meneja wa Jiji la Kisumu Abala Wanga amezitaka kampuni za utangazaji kufuata utaratibu unaostahili wakati wa kuweka mabango.  

Wanga alisema hawajui taratibu zozote za kisheria zinazofuatwa katika kuweka bango hilo.

Aliitaka kampuni husika kutoa nyaraka zinazoonyesha iwapo walifuata kanuni zilizowekwa za kuweka matangazo hayo.

(Utafsiri: Samuel Maina)