Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja Hakukamatwa - Polisi wasema

Muhtasari
  • Msemaji wa polisi, Bruno Shioso, alisema kuwa Sakaja alijiwasilisha kwa makao makuu ya DCI kufuatia ripoti za awali kuwa alikuwa anachunguzwa
Johnson Sakaja,baada ya kujiwasilisha katika makao makuu ya DCI

Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) inasema Seneta wa Nairobi, Johnson Sakaja, hakukamatwa kama ilivyoripotiwa awali.

Msemaji wa polisi, Bruno Shioso, alisema kuwa Sakaja alijiwasilisha kwa makao makuu ya DCI kufuatia ripoti za awali kuwa alikuwa anachunguzwa.

"Seneta alijiwasilisha katika Makao Makuu ya DCI kufuatia ripoti za awali za magazeti kwamba alikuwa akisakwa na polisi kuhusu suala la shahada ya chuo kikuu lililoimbwa na mahakama na taratibu za uchaguzi," Shioso alisema katika taarifa.

Shioso aliongeza kuwa Sakaja "alipokelewa kwa ukarimu na maafisa na akarudishwa kwa kuwa hakuwa ameitwa. Kwa hiyo aliondoka bila hatua zozote za polisi."

Seneta wa Nairobi, Johnson Sakaja, alijisalimisha kwa polisi Ijumaa, Juni 17, baada ya ripoti kuwa anachunguzwa kuhusu shahada yake ya Uganda.

Sakaja alijiwasilisha kwa makao makuu ya DCI kando ya Barabara ya Kiambu ili kuhojiwa. Mawakili wake walipiga kambi nje ya makao makuu ya DCI baada ya kunyimwa kuingia.

Kabla ya kujisalimisha, Seneta huyo wa Nairobi, ambaye anawania wadhifa wa ugavana wa jiji hilo, alizozana vikali na mkuu wa DCI, George Kinoti, akimtaka kumkamata.