Ruto - Mashujaa wa Kampeni yetu walikuwa mama mboga na watu wa Bodaboda

Ruto pia alisema kwamba mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alikuwa shujaa wa uchaguzi.

Muhtasari

• Rais mpya wa Kenya amewasifia watu wa maisha ya kipato cha kadri kwa kusema kwamba wao ndio walikuwa mstari wa mbele katika kampeni zake kuhakikisha ushindi wake.

Rais mteule William Ruto amewashukuru watu wa maisha ya ngazi za chini
Rais mteule William Ruto amewashukuru watu wa maisha ya ngazi za chini
Image: Facebook

Rais mteule William Ruto amewashukuru wote waliokuwa wakimenyana naye katika kinyang’anyiro cha urais wakiwemo mhubiri David Mwaure, wakili George Wajackoyah na mshindani wake mkuu Raila Odinga kwa kile alisema kwamba hawakuwa maadui bali walimenyana ili kuonyesha demokrasia komavu ya Kenya.

Ruto alikuwa akizungumza katika hotuba yake ya shukrani baada ya mahakama ya upeo kuidhinisha ushindi wake na alidokeza kwamba baada ya hapo angewapigia simu wapinzani wake wote ili kuwapongeza kwa kudumisha utulivu na amani wakati huu wote tangu kampeni, uchaguzi na kesi ikiendelea katika mahakama.

Ruto pia alisema kwamba atampigia simu rais anayeondoka Uhuru Kenyatta  ili kuzungumza naye na kusisitiza kwamba bado hajazungumza naye.

“Hivi karibuni nitampigia rafiki yangu rais Uhuru Kenyatta simu. Bado sijaongea na yeye,” Ruto alisema.

Rais  mteule pia aliwatambua wananchi wa kawaida - hustlers na kusema kwamba ushindi wake uliwezeshwa pakubwa na watu hao ambao wengi kwa jina la jumla wanajulikana kama mama mboga na watu wa boda boda.

“Mashujaa wa kampeni hii ni mama mboga na watu wa boda boda. Shujaa wa uchaguzi ni Wafula Chebukati,” Ruto alisema.