Aliyekuwa Mbunge wa Kesses Dkt. Kiprop Swarup Mishra amewaomba wapiga kura wa eneo bunge hilo kumsamehe kwa kutojiunga na Chama cha William Ruto cha UDA katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 uliokamilika.
Kulingana na runinga ya NTV, Mishra ambaye alipoteza azma yake ya kutetea kiti cha ubunge cha Kesses alisema hana lolote la kibinafsi dhidi ya Rais mteule na kwamba hatua yake ni upotoshwaji wa kisiasa ambao alifanyiwa na baadhi ya watu waliomshauri vibaya na kuishia kupoteza kiti hicho
"Ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa kwa jamii yangu kunisamehe kwa uamuzi niliochukua na nikakosea mwisho wa siku. Wakati mwingine kwa sababu ya kutokuwa na hekima, uamuzi mbaya unaweza kutokea na ni muhimu kujirekebisha ili isijirudie," mbunge huyo alisema.
Mishra alikuwa akiwania kama mgombeaji huru na akashindwa na Julius Rutto ambaye alikuwa akigombea kwa tiketi ya UDA.
Mishra pia alituma ujumbe wa nia njema kwa Dkt Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua akisema katika uongozi wao hana hofu wala wasiwasi kwamba wataliongoza taifa kurudi katika uchumi wake wa awali na hata kusonga mbele zaidi.
“Mimi na familia yangu tungependa kuwasilisha pongezi zetu za dhati kwa rais mpya, Dkt. William Ruto, na kumtakia mafanikio katika jina la Mungu. Mheshimiwa, ninafahamu kikamilifu ukubwa wa kazi iliyo mbele yako na nina imani kuwa chini ya uongozi wako, Kenya itatafuta njia mwafaka za kutatua changamoto zinazokabili nchi yetu,” Mishra aliongeza kwa kuandika kwenye Twitter yake.
Chama cha William Ruto cha UDA kilinyakua viti vya kuchaguliwa katika eneo kubwa la North Rift ambalo linachukuliwa kuwa ngome ya Ruto.
Kando na Mishra, wabunge wengine wa sauti waliopoteza ombi lao kwa wawaniaji wa UDA ni Alfred Keter huko Nandi Hills, Vincent Tuwei huko Mosop, Cornelly Serem huko Aldai, na Dkt James Murgor huko Keiyo Kaskazini.
Rais mteule William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua wanatazamiwa kuapishwa Jumanne, Septemba 13 katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi na inatarajiwa rais anayeondoka Uhuru Kenyatta atahudhuria ili kukabidhi madaraka licha ya tofauti zake za kisiasa na Ruto.