logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Tunashindana na timu iliyotamauka, kuweni macho! - Ruto awaambia Kenya Kwanza

"Watu wanaoweza kutumia Kamati ya Usalama kujaribu na kupindua matakwa ya watu wanaweza kufanya vibaya zaidi." - Ruto

image
na Radio Jambo

Habari08 September 2022 - 07:15

Muhtasari


Kuweni makini, wanaweza kuwakamata baadhi yenu ili tu kupunguza idadi yetu - Ruto.

Rais mteule William Ruto jana alikuwa na kikao cha viongozi wote waliochaguliwa kupitia vyama tanzu vya Kenya Kwanza katika makazi yake rasmi eneo la Karen, Nairobi.

Viongozi waliochaguliwa kama wabunge na maseneta wanatarajiwa kuapishwa Alhamisi leo hii na baadae kushiriki kura ya kuwachagua maspika na manaibu spika katika majumba yote mawili.

Katika hotuba yake, Ruto aliwaonya viongozi hao dhidi ya kutorubuniwa kwa mlungula ili kupiga kura yao kwa mgombea uspika na naibu spika kutoka mrengo wa Kenya Kwanza huku akisema kwamba ana habari mrengo wa upinzani una njama ya kutumia kila mbinu ili kulemaza idadi ya Kenya Kwanzan bungeni na hivyo kushinda uspika kwa kura nyingi.

Ruto alisisitiza kwamba wapinzani wao wakiongozwa na mwenyekiti wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Uhuru Kenyatta baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha urais, ni watu waliotamauka sana na wanaweza kutumia njia yoyote ili kuhakikisha wanapata viti vya maspika na manaibu yao katika seneti na bunge la kitaifa.

Kutokana na hilo, Ruto aliwasihi na kuwaonya viongozi wa Kenya Kwanza kuwa macho ili kukwepa mitego yote itakayolenga kusambaratisha idadi yao.

“Tunashindana na timu iliyokata tamaa sana. Watu wanaoweza kutumia Kamati ya Usalama kujaribu na kupindua matakwa ya watu wanaweza kufanya vibaya zaidi. Wanatamani sana kuwa na Spika wa Bunge lolote lile. Kuweni makini, wanaweza kuwakamata baadhi yenu ili tu kupunguza idadi yetu lakini tusichukulie jambo lolote kirahisi,” Ruto aliwashihi.

Katika bunge la Kitaifa, Kenya Kwanza imemuidhinisha seneta wa Bungoma Moses Wetangula kuwania uspika huku kwenye bunge la seneti, aliyekuwa gavana wa Kilifi Amason Kingi akiwania kama spika.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved