(+video) Waziri Omamo atokwa na machozi kumpa rais Kenyatta kwaheri

Raychelle Omamo alikuwa waziri wa ulinzi miaka 7 kutoka 2013 kabla ya kuhamishwa kwenda wizara ya mambo ya kigeni.

Muhtasari

• Itakumbukwa Omamo ndiye mmoja wa mawaziri ambao waliazna kazi katika utawala wa Uhuru Kenyatta kipindi chake cha kwanza kilipong’oa nanga mwaka 2013.

Jana idara ya majeshi ya ulinzi iliandaa sherehe ya mwisho ya kumpa kwaheri rais anayeondoka Uhuru Kenyatta katika uwanja wa Ulinzi Complex, Lang’ata jijini Nairobi.

Hii ilikuwa hafla ya mwisho kabisa ya kumtambua Kenyatta kama mkuu wa majeshi huku uongozi wake ukikaribia ukingoni na rais mpya William Ruto kuapishwa rasmi kama rais wa tano Jumanne Septemba 13.

Katika hafla hiyo ya kijeshi, mawaziri mbali mbali waliokuwa katika serikali ya Jubilee walionekana kutoa jumbe za kugusa mno na wengine kuzidiwa na hisia mpaka kutokwa na machozi.

Sasa kwenye mtandao wa Twitter, kumezuka klipu moja ya video inayomuonesha Waziri Raychelle Omamo akitokwa na machozi kwa kuzidiwa na hisia kutokana na kuondoka kwa rais Kenyatta kama mkuu wa majeshi.

Omamo ambaye ni Waziri wa masuala ya nje alionekana akijifuta machozi kwa hanchifu huku akielekea kwenye ukumbi mkuu pamoja na watu wengine wenye hadhi katika serikali ya Kenyatta kumsubiri.

Alijikaza na kupanda ukumbini huku machozi yanamlenga na kujiunga na baadhi ya mawaziri wenzake waliokuwemo, Dkt Fred Matiang’i wa usalama wa ndani, Eugine Wamalwa wa ulinzi miongoni mwa wengine.

Klipu hiyo imezungumziwa sana huku baadhi wakimtetea Omamo kwa kuzidiwa na hisia kwani si rahisi kutengana na mtu ambaye amekupa kazi kwa zaidi ya miaka 10.

Itakumbukwa Omamo ndiye mmoja wa mawaziri ambao waliazna kazi katika utawala wa Uhuru Kenyatta kipindi chake cha kwanza kilipong’oa nanga mwaka 2013.

Kazi yake ya kwanza chini ya utawala wa rais Kenyatta ilikuwa Waziri wa ulinzi ambapo alikipiga kwa miaka 7 kabla ya kubadilishwa kupelekwa wizara ya masuala ya nje huku aliyekuwa Waziri wa ugatuzi Eugine Wamalwa akikabidhiwa wizara ya ulinzi mpaka leo.