Mimi sio mtu wa kichini chini, Nikitaka kukutana na Ruto naweka wazi - Kalonzo

Kalonzo pia alimpongeza Ruto kwa ushindi na kusema yeye atahudumu kama mpinzani wa serikali.

Muhtasari

• Kiongozi huyo wa Wiper alisema yeye anafurahia kuhudumu kutoka upinzani na wala hajakutana na Ruto.

• Alisema picha zinazosambazwa akiwa nac Ruto ni za 2018 alipopoteza babake.

Kalonzo Musyoka wakilonga na William Ruto
Kalonzo Musyoka wakilonga na William Ruto
Image: Maktaba

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amepuuzilia mbali uvumi kwamba yumo mbioni kujiunga mrengo wa serikali unayoongozwa na rais mteule William Ruto.

Akizungumza Jumamosi, Kalonzo aliapa kwamba yeye atasalia kwenye mrengo wa upinzani ili kupambana vilivyo na serikali ya Dkt. Ruto.

“Siwezi jali hata kama tutakuwa kwa upinzani, tutasukuma. Tutashinikiza ili bwawa la Yatta litengenezwe na miradi mingine. Hata itakuwa vizuri zaidi kwangu nikiwa upinzani ili kung’ang’ana na watu hawa. Huwa tunasema miaka 5 ni kipindi kifupi sana na tumejitolea kuhudumia Wakenya kutoka upinzani kwa njia mwafaka kulingana na uwezo wetu, na tuko tayari” Kalinzo alisema.

Kiongozi huyo ambaye alikuwa makamu wa rais Kibaki alichukua pia fursa hiyo kumpongeza Ruto na kusema kwamba wanamheshimu licha ya kutokubaliana na matokeo ya kesi ya mahakama ya upeo Jumatatu.

Alipinga vikali madai yanayomhusisha na kushikana mikono na rais mteule William Ruto na kusema kwamba kiongozi huyo wa UDA alikwenda kumuona wakati mmoja alipopoteza babake mzazi na kusema hawana urafiki wa karibu na yeye kama ambavyo imekuwa ikisemekana mitandaoni.

“Kuna wengine walikuwa wanaweka kwa mitandao picha tukiwa na Ruto wakisema Kalonzo amekutana na Ruto. Alikuja kuniona wakati nilipoteza babangu 2018 na hizo picha ndio watu wanatumia mitandaoni. Mimi sio mtu wa kichini chini. Nikitaka kukutana na Ruto nitakutana na yeye wazi baada ya kufanya mazungumzo na chama chetu cha Wiper na Azimio la Umoja One Kenya,” aliongeza.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na mfumuko wa wanasiasa kutoka vyama vya upinzani kujiunga na mrengo wa Ruto na mwishoni mwa wiki jana uvumi ulisambazwa kwamba Kalonzo baada ya kujiondoa katika kinyang’anyiro cha spika wa seneti, yumo mbioni kujiunga na Ruto, jambo ambalo alilipuuzilia mbali kabisa Jumamosi katika hafla moja ya mazishi huko kwao Ukambani.