Omtatah aapa kupambana na jaji Lenaola kwa kumtishia na meseji WhatsApp

Alisema twende kazi na tutaenda kazi - Omtatah

Muhtasari

• Nimetetea ombi langu mbele yako, halafu unategemea kujitoa, rafiki yangu hapa hujitoi,” Omtatah alitema moto - Omtatah

Omtatah aapa kupambana na jaji Lenaola
Omtatah aapa kupambana na jaji Lenaola
Image: Maktaba

Seneta wa Busia Mwanaharakati Okiya Omtatah amefichua kwamba jaji Isaac Lenaola, mmoja wa jopo la majaji saba wa mahakama ya upeo alimtumia ujumbe wa kumtishia kwenye WhatsApp.

Omtatah alisema ujumbe huo ulikuja baada yake kudai kwamba jopo lile lilikuwa limeengemea upande fulani wakati wa kusikilizwa kwa maombi ya kesi iliyowasilishwa kutaka ushindi wa Ruto kubatilishwa.

Akizungumza kwenye runinga moja nchini usiku wa Jumatano, seneta huyo mpya kabisa alidokeza kwamba bado wangali kwenye vita na jaji huyo mpaka sasa kutokana na ujumbe huo ambao alisema ni wa vitisho dhidi yake.

Omtatah ambaye wengi wanamjua kutokana na hulka yake ya kuwasilisha kesi mahakamani kupinga baadhi ya sheria na maagizo ya serikali alisema kwamba kwa sababu jaji huyo alianzisha vita basin aye ni mzuri sana katika kujibu mipigo.

“Hata mmoja wa majaji hao tunapigana sasa hivi…Jaji wa Mahakama ya upeo alinitisha kwenye WhatsApp. Jaji Lenaola alinitisha…alisema twende kazi na tutaenda kazi. Mimi ni mpambanaji rafiki yangu, na katika hili tutapelekana mbio kweli,” Omtatah alisema.

Mwanaharakati huyo alionekana kusisitiza kwamba hii vita ndio mwanzo inaanza kwa kile alisema si jambo zuri kuja kutoka kwa jaji wa mahakama ya juu na katu jaji Lenaola hawezi akaondoka katika vita hiyo.

“Na ukizingatia kwamba hivi vitisho vilikuja kutoka kwa jaji wa mahakama ya upeo ambaye nimetetea ombi langu mbele yako, halafu unategemea kujitoa, rafiki yangu hapa hujitoi,” Omtatah alitema moto.

Okiyah Omtatah alisema ujumbe huo ndio unamfanya kufikiri kwamba kesi yake haikusikilizwa na kuamuliwa kwa njia sahihi.

Alikuwa amewasilisha kesi kweney mahakama hiyo akisema kwamba hakuna mgombea urais alifikisha asilimia 50+1 kama inavyohitajika kisheria na ombi lake lilitupiliwa mbali katika njia ambayo sasa anahisi haikuwa ya haki.