Marais wa Afrika walisafiria gari la kubeba maiti kuenda kuona maiti - Babu Owino

Mbunge huyo alikejeli hatua ya serikali ya Ruto kudai hakuna pesa huku akisafiri kwenda Uingereza na Marekani.

Muhtasari

• Marais wa Afrika walibebwa kwenye gari la kubebea maiti kwenda kumwona marehemu Malkia - Babu Owino.

Babu Owino akejeli hatua ya marais wa Afrika kusafiri Uingereza kwa mazishi ya malkia Elizabeth 2
Babu Owino akejeli hatua ya marais wa Afrika kusafiri Uingereza kwa mazishi ya malkia Elizabeth 2
Image: facebook

Mbunge wa Embakasi East Babu Owino amekuwa mtu wa hivi punde kuzungumzia suala la marais wa Afrika kusafirishwa kwa basi kuelekea eneo la hafla ya msiba wa malkia wa Uingereza, Elizabeth II.

Babu Owino katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, amemtupia kiazi moto kinywani rais William Ruto kwa kile alisema kwamba kuondoka Afrika ili kuelekea ughaibuni kuona maiti ni hulka ya kizamani.

Babu Owino alionekana kufurahia kitendo hicho amabcho marais wa Afrika walifanyiwa kusafirishwa kwa mkupuo katika basi moja.

Kulingana na mbunge huyo mkosoaji mkubwa wa serikali ya Ruto, haina haja mtu kusafiri kuenda Uingereza kuona maiti kwa sababu kuna kazi nyingi za muhimu huku nyumbani ambazo mtu anaweza akafanya.

Owino alimsuta Ruto na uongozi wake kwa kudai kwamba uongozi ulioondoka ulifyonza kila kitu kutoka kwa akaunti za serikali. Alisema kwamba kauli hizo ni uongo kwani haiwezekani waseme hakuna pesa kwenye akaunti ilhali wanaendelea kutumia hizo pesa kufanya ziara kote duniani.

“Marais wa Afrika walibebwa kwenye gari la kubebea maiti kwenda kumwona marehemu Malkia. Unaondokaje Kenya na matatizo yake yote kwenda kuona maiti London bado unadai kwamba hakuna pesa Kenya!!!Hustlers mtajionea mambo,” Owino aliandika.

Rais Kenyatta aliondoka wikendi iliyoita kuelekea Uingereza kushiriki hafla ya mazishi ya malkia Elizabeth wa pili akiongozana na mama Rachael Ruto.

Baadae ataondoka kuelekea Marekani kwa hafla ya 77 ya kongamano la umoja wa mataifa.