Si vibaya marais wa Afrika kubebwa kwenye basi, ni funzo - Miguna Miguna

Marais hao walionekana kusafiri ndani ya basi moja kuelekea msibani, jambo lililozua maoni kinzani mitandaoni.

Muhtasari

• Hakuna ubaya kwa marais na mawaziri wakuu wa Kiafrika kuchukua mabasi kwenda kwenye mazishi ya mfalme wa kikoloni na mbaguzi.

Miguna Migunsa aema si vibaya kwa marais wa Afrika kubebwa kwa basi Uingereza
Miguna Migunsa aema si vibaya kwa marais wa Afrika kubebwa kwa basi Uingereza
Image: TWITTER

Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza alizikwa jana katika hafla ambayo ilihudhuriwa na marais kutoka mataifa takribani 200 kote duniani.

Katika hafla hiyo ya msiba, kulizuka uvumi baada ya picha za marais wa Afrika kuonekana wakiwa ndani ya basi moja wakisafiri kuelekea eneo la mazishi.

Picha hizo zilizua ghadhabu kubwa mitandaoni huku watu haswa Waafrika wakiisuta serikali ya Uingereza kwa kuwabagua marais wao katika usafiri.

Ilisemekana kwamba marais wachache tu ndio waliruhusiwa kusafiri kwa magari yao binafsi huku wengi wao wakitakikana kutumia gari la pamoja ili kuepusha msongamano.

Nchini Kenya, baadhi ya viongozi akiwemo aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko walisuta Wazungu kwa kusema kwamba hatua ya kuwasafirisha marais wa Kiafrika kwenye basi moja ni dhuluma.

Sonko alisema kwamab wazungu hao hawana adabu na hata kuuliza wataeleza Watu nini kwa mfano kitu kibaya kikatokea kwenye basi hilo na kuwaangamiza marais hao wote.

Lakini kuna wengine ambao walionekana kutojali sana suala hilo na kusema kwamba ni jambo la kawaida kwa marais kusafiri ndani ya basi moja.

Wakili aliyeko uhamishoni, Miguna Miguna ni mmoja wa kundi la mrengo ulioonekana kutojali sana hatua hiyo kwa kile alisema kwamba ni jambo la kawaida tu marais kusafiri kwa gari la pamoja.

“Hakuna ubaya kwa marais na mawaziri wakuu wa Kiafrika kuchukua mabasi kwenda kwenye mazishi ya mfalme wa kikoloni na mbaguzi. Ni jambo sahihi kufanya. Nzuri kwa walipa kodi. Bora kwa mazingira. Na somo la makata dhidi ya utajiri chafu,” Miguna Miguna alitoa maoni yake kwenye mtandao wa Twitter.