Mwigizaji Lijodi aomba msaada wa matibabu kwa mwanawe anayeugua Sickle Cell Anaemia

Gharama ya matibabu ni kiasi cha Ksh. 625,275 - Kokoto aliandika.

Muhtasari

• Ninatoa wito kwa kila mmoja wenu kusimama nami katika jambo hili kubwa - Kokoto.

• Alisema mwanawe anafaa kusafirishwa kwenda India kwa matibabu hayo.

Mwigizaji Lijodi Kokoto aomba msaada kwa matibabu ya mwanawe
Mwigizaji Lijodi Kokoto aomba msaada kwa matibabu ya mwanawe
Image: instagram

Aliyekuwa mwigizaji wa kipindi cha ucheshi cha Vioja Mahakamani Lijodi Kokoto ameelezea matukio ya kusikitisha mno kuhusu afya ya mwanawe.

Mwigizaji huyo ambaye pia anajiongeza kama mtangazaji wa redio alisema mwanawe kwa muda mrefu sasa amekuwa akiishi na ugonjwa wa seli Mundu, almaarufu Sickle Cell Anaemia kwa kimombo.

Alielezea kwa upana kupiti ukurasa wake wa Instagram na kusema kwamba tatizo hilo limeifilisisha familia kwa kujaribu mbinu zote kumpeleka hospitali mtoto wao kila mara.

“Labda umesikia ugonjwa wa mwanangu. Ndiyo. Wesley Obama alipatikana na ugonjwa wa Sickle Cell (SCD) - ugonjwa unaohusiana na damu. Mara kwa mara, tumekuwa tukifanya kazi bila kuchoka ili kumwona ndani na nje ya hospitali,” Lijodi alisema.

Mwigizaji huyo aliwaomba msaada wasamaria wema na watu wenye moyo wa kutoa kumsaida ili kusimamia gharama ya matibabu ambayo mpaka sasa inasoma zaidi ya laki sita pesa za benki kuu ya Kenya.

“Gharama ya matibabu ni kiasi cha Ksh. 625,275. Hivi sasa, Mimi na familia hatuko katika nafasi ya kumudu kiasi hiki na kwa kuzingatia ratiba iliyotolewa na madaktari (matibabu yafanyike mwisho wa Agosti). Ninatoa wito kwa kila mmoja wenu kusimama nami katika jambo hili kubwa. Wesley anapaswa kusafirishwa hadi India kwa matibabu,” Kokoto aliomba.

Aliwataka mashabiki wake wote kando na kusimama na mwanawe kwa michango pia wamkumbuke katika maombi pamoja pia na watu wote ambao wanapitia tatizo la kiafya kama hilo.

Kwa kuweka ubinadamu mbele ya kitu chochote kile, Lijodi amewaomba wenye moyo wa kutoa kupeperusha miamala kwa Nambari ya Paybill 8048537, Jina la Akaunti : Wesley Obama (mgonjwa)