Hii si ya mwisho, tutakuwa tukifanya ibada Ikuluni mara kwa mara - Mama Rachael Ruto

Mama wa taifa alikuwa akiyazungumza haya katika ibada maalum iliyoandaliwa kwenye ikulu ya Nairobi wikendi iliyopita

Muhtasari

•Mama wa Taifa alisema kuwa miaka baada ya miaka watu watakuwa wakienda Ikuluni kwa siku ya shukrani.

Image: HISANI

Mama wa Taifa Rachael Ruto, kwenye ibada ya kanisa iliyoandaliwa katika ikulu ya Nairobi, alitangaza kuwa kutakuwa na ibada za mara kwa mara katika kila mwezi kwenye makazi hayo rasmi ya rais na familia yake.

Alisema na kuwaambia viongozi wa kanisa kuwa watakuwa wakiitembelea Ikulu ili kuandaa ibada ya kurudisha Shukrani kwa  Mwenyezi Mungu shukrani.

“Hii si misa ya mwisho tutakayoweza kuwa nayo Ikuluni, unapobarikiwa na kujibiwa ombi lako, unampa Mungu shukrani,kwa hakika uamsho umefika” alisema.

Alisema alihisi kuwa milango yake imefunguka na alimshukuru Rais kwa kuwakubali watumishi kuandaa ibada hiyo ikuluni na pia kuweka maombi.

Mama wa Taifa alisema kuwa miaka baada ya miaka watu watakuwa wakienda Ikuluni kwa siku ya shukrani.

“Nataka kuichukua fursa hii kushukuru kanisa kwa kuiombea nchi hii, kila kitu kinachozaliwa kwa maombi kinapaswa kutegenezwa kwa maombi,” alisema.

Mama Rachel pia alisema kuwa watazidi kumpa Mola shukrani na si mara moja ila mara kadha wa kadha.

Aliwashukuru watumishi wakuu na kuwaambia kuwa Kanisa ndilo litakalo ipeleka nchi ya Kenya kwenye kiwango kingine.

Hii ni baada ya Rais William Ruto kuwasili nchini kutoka Marekani alipokuwa amehudhuria Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuandaa misa ile katika ikulu ya Nairobi.

Ibada hiyo iliandaliwa katika Ikulu ya Nairobi ndiyo ya kwanza kufanyika kutoka uapisho wake Rais na baada yake kuhamia kule Ikuluni. Iliwakutanisha viongozi mbali mbali wa Kikristo waliojumuika kufanya maombi maalum.

Rais alisema aliandaa ibada ile ili kuombea uchumi wa taifa la Kenya unaodorora kufuatia madeni mengi ambayo Kenya inadaiwa na mashirika mbali mbali ya kimataifa.

“Ombeeni uchumi wa Wakenya unaodorora. Tumefungamana na madeni yetu ambapo asilimia 65 ya ushuru tunaokusanya huingia katika kulipa madeni," Ruto alisema.