(+video) Wazazi wa Wendy walia kwa uchungu kando ya bwawa la kuogelea alikozama mwanao

Hellen Wendy, ni nesi aliyefariki akiwa anapeperusha moja kwa moja kwenye Facebook.

Muhtasari

• Mama Wendy aliyeumia moyoni alionekana akifarijiwa huku akiomboleza kwa maumivu huku akitazama sehemu ambayo binti yake alizama.

Mwezi mmoja uliopita dunia ilistaajabishwa na kisa cha msichana Mkenya aliyefariki baada ya kuzidiwa na maji kwenye bwawa la kuogelea nchini Canada.

Hellen Wendy, binti wa miaka 24 alikuwa ni nesi huku ughaibuni na alikuwa anapeperusha moja kwa moja kwenye mtandao wa Facebook akiogelea kabla ya kuzama huku marafiki na mashabiki wake wakimtazama mubashara wakishindwa cha kufanya kumsaidia asizame, haswa baada ya kusikika akiitisha msaada bila mafanikio.

Mwezi mmoja baadae, habari hizo zimeibuka tena huku video zikionesha familia yake hatimaye imewasili Canada tayari kwa kuchukua mwili wake na kurudi kuuzika nyumbani kwao katika kaunti ya Kisii.

Familia hiyo ikiongozwa na babake na mamake walifika Canada na kutembelea bwawa lile la kuogelea ambako mpendwa wao alipoteza maisha na kufanya matambiko ya rambi rambi zao kwa majonzi na huzuni mwingi.

Katika video mitandaoni, wazazi hao waliokuwa wamehuzunika walionekana wakilia kando ya bwawa hilo. Mama Wendy aliyeumia moyoni alionekana akifarijiwa huku akiomboleza kwa maumivu huku akitazama sehemu ambayo binti yake alizama majini na kupoteza maisha pasi na msaada wowote kutoka kwa waopoaji.

Mwezi mmoja uliopita baada ya taarifa hizo za tanzia kugonga vichwa vya habari kote ulimwenguni, babake alisema kuwa binti huyo nesi ndiye alikuwa tegemeo kwa familia yao na hata alikuwa anasaidia kuwasomesha ndugu zake wadogo.

Video hiyo yenye hisia imetia wengi huruma mitandaoni baadhi wakisema kwamba uchungu ambao wanafamilia hao wanapitia haswa wazazi wake si kitu ambacho mtu anaweza kumtakia hata adui yake namba moja.

Ama kweli, mzazi hafai kabisa kumzika mwanawe, ni uchungu usioweza kumithilika kwa mizani ya dunia hii!