logo

NOW ON AIR

Listen in Live

EACC yazindua uchunguzi kuhusu wizi unaoshukiwa wa Ksh.196M ​ katika kaunti ya Isiolo

EACC ilidokeza kuwa Kaunti ya Isiolo ni mojawapo ya kaunti nyingi zinazokabiliwa na ufujaji wa pesa

image
na Radio Jambo

Habari28 September 2022 - 18:46

Muhtasari


  • Wakati wa uchunguzi wa awali, Tume ilibaini kuwa malipo hayo yalifanywa kwa tarehe tofauti kati ya 2019 na 2022
  • Hii itajumuisha kutoa ufikiaji wa hati zinazohitajika, pamoja na hati za malipo zinazohusika
Picha ya makao makuu ya EACC jijini Nairobi

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeanzisha uchunguzi kuhusu upotevu wa pesa za umma  Sh196,016,910 katika Kaunti ya Isiolo.

EACC ilisema pesa hizo ni malipo ya ulaghai yaliyofanywa kwa akaunti za benki za maafisa watano katika Idara ya Fedha na Mipango ya Kiuchumi ya Serikali ya Kaunti.

Wakati wa uchunguzi wa awali, Tume ilibaini kuwa malipo hayo yalifanywa kwa tarehe tofauti kati ya 2019 na 2022.

EACC inashuku kuwa pesa hizo zilihamishiwa kwenye akaunti, ili zigawe baadaye miongoni mwa maafisa wengine wakiwemo wale wa uongozi mkuu wa kaunti.

Kiasi cha fedha kilichopokelewa na kila mmoja wa viongozi hao katika kipindi cha miaka minne ni pamoja na Sh48,697,530, Sh30,452,715, Sh46,971,100, Sh20,432,965 na Sh49,462,600.

Tume imeiandikia Serikali ya Kaunti, kupitia Katibu wa Kaunti, kusaidia katika uchunguzi huo.

Hii itajumuisha kutoa ufikiaji wa hati zinazohitajika, pamoja na hati za malipo zinazohusika.

“Kukosa kuwasilisha stakabadhi zinazohitajika kwa uchunguzi wa ufisadi ni kosa chini ya Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi, 2003,” EACC ilisema.

EACC ilidokeza kuwa Kaunti ya Isiolo ni mojawapo ya kaunti nyingi zinazokabiliwa na ufujaji wa pesa za kaunti.

"Changamoto hii inaashiria uangalizi hafifu wa Mabunge ya Kaunti ambayo yameanzishwa, miongoni mwa majukumu mengine, kuhakikisha uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma kupitia uangalizi mzuri," shirika la kupambana na ufisadi lilisema.

Tume ilihimiza Mabunge kuzingatia majukumu yao na kuimarisha usimamizi wao wa matumizi ya rasilimali za umma na maafisa wakuu wa kaunti.

EACC pia iliwataka Magavana kusaidia kukomesha ufisadi kwa kuondoa mzozo wa maslahi katika shughuli za kaunti na kusambaratisha mitandao yoyote iliyopo ya ufisadi.

 

 


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved