Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko hatimaye alikutana na mridhi wake Anne Kananu kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu.
Wanasiasa hao walikutana Jumanne jioni katika eneo lisilofichuliwa na kushiriki vinywaji pamoja. Mahasidi hao wa zamani pia walishiriki mazungumzo pamoja.
Sonko ndiye aliyefichua habari za kikao hicho kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii na kudokeza kuwa kiliweza kumaliza uadui wao.
"Hakuna uadui wa kudumu kwenye siasa, sasa tukumbatiane kwa kwenda mbele," alisema mfanyibiashara hiyo.
Kananu alichukua usukani kama gavana wa tatu wa Nairobi mnamo Januari 2021 baada ya Sonko kubanduliwa. Alipata kibali cha kumrithi Sonko mnamo Novemba 9, 2020 baada ya Mahakama ya Juu kutupilia mbali ombi la kupinga uteuzi wake.
Mwezi Januari 2020, Sonko alimteua Kananu kama naibu wake na kuwasilisha jina lake kwa bunge la Kaunti ili kuhakikiwa.
Hata hivyo kabla ya bunge kumhakiki, kesi iliwasilishwa mahakamani kupinga uteuzi wake na kupelekea agizo la mahakama kusimamisha bunge kutoendelea na uhakiki na kumuidhinisha kama naibu gavana.
Hatima ya Kananu ilibaki kitendawili hadi Desemba 2020 wakati Sonko alipotimuliwa madarakani na mahakama hatimaye ikaondoa amri iliyozuia bunge la Nairobi kumhakiki na kuidhinisha uteuzi wake.
Baadaye alihakikiwa, akaidhinishwa, na kuapishwa kama naibu gavana lakini alipokuwa akijiandaa kuchukua wadhifa wa ugavana, Sonko akakimbia mahakamani na kuomba kusitisha kiapo hicho.
Baadae mahakama kuu ilitupilia mbali ombi la Sonko na kuandaa mazingira ya kuapishwa kwa Kananu kama gavana.
Tangu Kananu kuchukua usukani wa Nairobi kumekuwa na uhusiano usio mzuri kati yake na aliyekuwa mtangulizi wake.