Wikendi iliyopita, mwenyekiti wa klabu cha soka cha Gor Mahia Ambrose Rachier alikuwa gumzo kubwa baada ya kufichua kwamba amekuwa kwenye kundi linalohusishwa na ushirikina wa kishetani, Freemason.
Kufuatia kufunguka huko, watu mbali mbali wamemjia juu kuuliza maswali kuhusu kundi hilo haswa pale aliposema kuwa azimio lao kuu ni kufanya hisani katika jamii.
Rachier alikanusha dhana inayohusisha kundi hilo na kuwapa watu utajiri pindi wanapojiunga nao na kusema kwamba wanachokifanya ni ihsani tu ili kuwakimu kimaisha wanachama wake.
Matamshi haya ndiyo yamemfanya wakili aliye uhamishoni Miguna Miguna kucharuka na kumzomea vikali Rachier kwa kusema kwamba yeye mwenyewe anatoka katika kijiji chenye kimerambwa na umaskini mbele nyuma, juu chini.
Miguna Miguna aliuliza maswali kuwa iwapo ni kweli Freemason inafanya hisani kwa watu, mbona basi haijasaidia watu kukwepa umaskini katika kijiji cha Rachier ambaye ni mwanachama wao kwa miaka 28.
Pia aliraka kujua hiyo hisani imemfanya Rachier kujenga shule au hata hospitali ngapi katika eneo la kijiji chake huko Siaya kama kweli dhumni kuu la Freemason ni kucheza katika nafasi ya msamaria mwema katika uwanja wa maisha.
“Ambrose Rachier anatoka katika eneo la Gem maskini katika Kaunti ya Siaya. Ikiwa FREEMASONS ni mabingwa wa hisani, je wamejenga shule ngapi, hospitali, vituo vya watoto yatima na walala hoi? Rachier amefadhili masomo kwa watu wangapi? ALIUA Gor Mahia kwa ibada yake ya shetani,” wakili Miguna Miguna alitupa bomu la moto kwenye kichwa cha Rachier.
Awali pia mshirika mwenza katika kampuni ya mawakili ya Rachier & Amollo Advocates, mbunge wa Rarieda Otiende Amollo alijitenga na uwezekano wake kuwa katika Freemason na Rachier.