Junamme alasiri kulikuwepo na mjadala mkubwa katika bunge la Kitaifa wakati wa kikao cha kwanza kabisa cha wabunge hao ambao wabunge walikuwa wanazungumzia kuhusu chama au muungano wenye wabunge wengi bungeni.
Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro ambaye ni mwandani mkubwa wa rais William Ruto alikuwa anazu ngumza wakati wa zamu yake ambapo alikuwa anawasuta wanachama wa muungano wa upinzani dhidi ya kuzua mjadala huo kwa kile alisema ilikuwa wazi Kenya Kwanza na haswa chama chao cha UDA ndio walio na wingi wa wabunge.
Katika tukio lisilo la kawaida na ambalo limezua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii, mbunge wa Gem Elisha Odhiambo aliomba spika Wetang’ula nafasi na kumkatisha Nyoro kauli yake.
Odhiambo alisimama na kumrekebisha Nyoro kwamba hakuwa ametumia mtiririko wa maneno katika lugha ya Kiingereza kwa njia inayofaa na kumtaka kuzungumza Kiingereza kilichokwenda skuli kama mheshimiwa.
“Nikiwa mmoja wa wabunge mashuhuri kutoka Gem, nataka nikukumbushe ndugu yangu fonetiki usiyoweza kuitumia; lazima uwe wazi kwenye lugha. Ongea Kiingereza Kizuri," Odhiambo alisema huku wabunge wenzake wakipasua vicheko.
Hata hivyo, hili halikumzuia au kumfanya Nyoro kujihisi kukandamizwa kwani aliendelea kutoa wasilisho lake huku akisema kuwa hakuwa na muda wa kujibu wala kufuata ushauri huo wa mbunge Odhiambo kwa kile alisema kuwa ni maneno yasiyo na misingi yoyote.