Wafanyikazi katika Mamlaka ya Kitaifa ya barabara kuu nchini Kenya, KeNHA wamefurahisha watu wengi kwenye mtandao wa Tweeter baada ya mamlaka hiyo kupakia msururu wa picha ikiwaonesha wakionesha ukarimu kwa madereva wa malori.
Ikumbukwe wiki hii imekuwa ni ya kusherehekea wateja katika sekta zote zinazohusisha biashara na huduma mbali mbali na KeNHA hawakuachwa nyuma kunyoosha mkono wao wa ukarimu kwa wateja wao ambao ni madereva.
KeNHA kupitia ukurasa wao wa Tweeter walipakia picha hizo zikiwaonesha wafanyikazi wao kwa furaha na tabasamu ghaya wakisambaza maji ya chupa kwa madereva wa malori ya kusafirisha bidhaa mbali mbali kwenye barabara.
“Wafanyakazi wa KeNHA pamoja na Axle Load Enforcement & Highway Unit (ALEHU) na timu ya usimamizi wa Weighbridge (ECWLtd) walisambaza maji ya kunywa kwa madereva wa malori katika mizani ya kupima uzito wa malori huko Mlolongo na Juja katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja. #kenhakuadhimisha,” KeNHA waliandika kwenye Tweeter huku wakifuatisha kwa picha kadhaa.
Mamlaka hii iliasisiwa mwaka wa 2008 na serikali ya nusu mkate ya hayati rais Mwai Kibaki pamoja na Raila Odinga kama taasisi mojawapo ya kushughulikia miundo mbinu nchini Kenya kuelekea ruwaza ya mwaka 2013.