Steve Oloo ni kamanda wa polisi katika kaunti ya Nyeri ambaye amegeuka gumzo mitandaoni haswa baada ya hotuba yake kwa wakaazi wa kaunti hiyo siku ya Mashujaa.
Katika hotuba yake ambayo imezua vichekesho, kamanda huyo aliwataka watu kuishi kwa Amani katika jamii ili kuepuka visa vya vurugu na fujo katika boma zao.
“Tukae kwa Amani, kwa nyumba zetu, na kwa jamii mahali tunaishi. Kama tumekosana, tukae pamoja, tuzungumze kwa sababu mahali Amani iko, kiukweli kutakuwa na utulivu,” Oloo alisema.
Pia alizidi kugusia suala la migogoro katika ndoa, akisema kwamba vurugu nyingi hutokana na wanadnoa kunyimana unyumba, aliwasihi wanawake kutekeleza wajibu wao katika kuwapa unyumba mabwana zao na kama hawajihisi basi wazungumze ili kupata mwafaka katika suala hilo.
“Kwa nyumba, mama ukiombwa unyumba, peana. Lakini ukijihisi umechoka, baba ukisikia mama amekuambia amechoka, kubali kwamba hajisikii na hata kesho ni siku utapata unyumba kwa sababu ni haki yako. Isije ikatokea kwamba umenyimwa unyumba ukaua mke au ukachukua Kamba kujiua,” Oloo aliwashauri wanaume pia.
Aliwataka wanaume kupunguza hasira pindi wake zao wanawakatalia unyumba na kuwaambia kwamba hasira zikiwaendekeza kuchukua maamuzi magumu ya kujiua basi wajue ni wao watapoteza kwa sababu wanawake bado watabaki na watapata unyumba kwingine.
Ushauri huu wa kamanda Oloo unakuja siku moja tu baada ya utafiti kufichua kwamba migogoro mingi katika ndoa na hata idadi kubwa ya visa vya talaka hutokea kwa misingi ya wanandoa kuchepuka au kunyimana unyumba.