Kiongozi wa chama cha Roots, wakili msomi George Wajackoyah Jumatatu alikuwa anasherehekea siku yake ya kuzaliwa, akifikisha miaka 63.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Wajackoyah aliweka hayo wazi huku akiwataka watu kutomtumia maua wala jumbe za heri njema, katika kile ambacho alionekana kudokeza kuwa amezoea.
“Leo ni siku yangu ya kuzaliwa. Hakuna maua au jumbe za heri njema,” Wajackoyah aliandika.
Licha ya kukataa, mamia ya Wakenya walifurika kwenye chapisho hilo na kumtakia heri njema ya siku yake ya kuzaliwa, huku wengine wakimuuliza mbona hataki salamu za heri njema na tayari ashawataarifu watu.
“Ningekumiminia jumbe za heri njema sana ili ufurahie furaha yako, lakini sasa unaposema "HAPANA" kwa salamu za heri njema, fanya bidii kuhakikisha kwamba nisikose katika sherehe ya keki. Niko Kisii🙂” mmoja kwa jina Anthony Kamau alimtania.
Hivi majuzi, Wajackoyah alitangaza kuwa amechukua nafasi ya upinzani kirasmi na kuwa atabaki pale ili kuhakikisha anaumlika uongozi wa rais Ruto kwa njia iliyo kamilifu.
Pia alimtaka kiongozi wa ODM Raila Odinga kumuunga mkono na kustaafu kabisa kutoka siasa kwani wakati wake umefika.
Wajackoyah alimaliza wa tatu kwa kura zisizozidi laki moja katika uchaguzi mkuu uliopita, uchaguzi ambao Ruto aliibuka mshindi kwa kumbwaga mpinzani wa karibu Raila Odinga aliyekuwa akiwania kutoka mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya.
Wajackoyah alidokeza kwamba huenda akawa debeni kujaribu kuingia ikulu tena katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2027, na kumtaka Raila kumuunga mkono wakati huo utakapofika.