Rais William Ruto aliwawakumbuka waliojeruhiwa pamoja na kijana mmoja aliyefariki katika mshikemshike ya kanisani eneo la Kenol miaka miwili iliyopita wakati wa kampeni zake.
Akizungumza katika kaunti hiyo ya Murang’a wikendi iliyopita, rais Ruto alisema kwamba kitendo cha polisi kutupa vitoza machozi kwa umati wa waumini ndicho kilichosababisha mkanyagano huo na kupelekea kijana mmoja kufariki huku wengine wakijeruhiwa.
Aliahidi kuwa hakuna siku hali kama hiyo itatokea katika kumbi za kuambudu tena na kusema kwamba baadhi ya watu wenye nguvu ya dola nchini walikuwa wamevimba vichwa kiasi cha kutoambilika wala kusemezeka.
Alisema kwamba hao watu wachache ambao walikuwa wameshikilia dola ndio walifanya njama ya kutupwa kwa vitoza machozi lakini sasa wamenywea na kunyenyekea, jambo ambalo alisema na matakwa ya Mungu kuwanyenyekesha wenye kiburi.
“Ndio ujue shetani alikuwa amekuwa kichwa ngumu hapa Kenya. Wanajuta mahali walipo kwa sasa. Hakuna siku vitoza machozi vitatupwa kanisani kwa madhabahu,” Rais Ruto alisema.
Naibu rais Rigathi Gachagua pia alizungumzia suala hilo na kusema kwamba wale polisi ambao walitumwa kutupa vitoza machozi katika mkutano huo wameshanyenyekea na hata wengine kuomba radhi kwa rais Ruto na naibu wake Gachagua.
“Polisi na maofisa tawala walioagizwa kukurushia mabomu ya machozi Maaskofu wetu walinifikia jana usiku na kuniomba msamaha maana walitumika vibaya na haikuwa nia yao kuleta fedheha,” DP Gachagua alisema.