Wanawake hawana huruma, pesa uliyopata kwa kutwanga matofali, bado anataka zote - Mgogo

Aliwaambia hata kama wanataka pesa lakini wawe wanauliza kama mwanaume huyo amemwachia kitu mkewe kabla ya kumkomba zote.

Muhtasari

• Mshahara wako ambao anajua una familia na watoto, anataka wote - Mgogo.

Mchungaji Daniel Mgogo
Mchungaji Daniel Mgogo
Image: Facebook//PastorDanielMgogo

Mchungaji maarufu kutoka Tanzania Daniel Mgogo amewataka wanawake wa kujiuza kuwa na huruma japo kidogo kwa wanaume wa watu ambao wanawachuna mpaka basi.

Kupitia klipu alichokipakia kwenye Instagram yake Jumanne alasiri, mchungaji Mgogo aliwashauri wanawake hao wa kujiuza kufahamu fika kwamba hata kama anatoka kimapenzi na huyo mwanaume, basi atambue kuwa ni mume wa mtu na ana familia vile vile inayomtegemea na hivyo kutomchuma mshahara wake wote.

“Sehemu zingine wanawake hawana huruma. Pamoja na pesa yako uliyoipata kwa kutwanga matofali, anataka yote. Mshahara wako ambao anajua una familia na watoto, anataka wote. Wakati mwingine niliwaambia na nyie wadangaji wwakati mwingine muwe na kahuruma kwa mbaali. Huyo mwanaume kweli umempata ni mume wa mtu, ni buzi lako ndio linakulipia pango la nyumba na kukufanyia kila kitu, lakini na wewe angalau huwe na huruma kuwa huyu ni mume wa mtu,” mchungaji Mgogo alishauri.

Mchungaji huyo aliwaambia kwamba kipindi buzi linaleta mshahara wote wanafaa kumuuliza kama kweli amemwachia mkewe kitu na wala si kuuparamia wote bila kujali.

“Anapoleta mshahara muulize mwenzangu umemwachia ngapi? Maana huyo ndio mke wako mimi ni jambazi tu. Yeye ndio anakuvulia nguo anakulelea watoto, mimi ni jambazi. Nigawie kidogo tu nyingine mpelekee dada,” Mchungaji Mgogo alitoa ushauri huku umati wa waumini ukipasua kicheko.

Pia aliwashauri wanaume kuwa na adabu katika kutumia pesa zao katika mambo ya kuwajenga na wala si kupata kidogo na kuzamia katika uzinzi.

“Wewe bado ndio unaanza maisha, uzinzi hapo hapo, ulevi hapo hapo, halafu unataka kuendelea, unafikiri wanawake watakuonea huruma?” aliwapa changamoto wanaume.