Samidoh apata ajali Marekani na kulazwa chumba cha matibabu ya dharura

Ajali hiyo ilimfanya kuahirisha ziara yake ya kimuziki aliyotarajiwa kutumbuiza eneo la Sponake, Marekani.

Muhtasari

• Ajali mbaya ilitokea asubuhi ya leo na kunipeleka kwa E.R , hivyo kutoweza kusafiri kwa onyesho la leo - Samidoh.

Samidoh apata ajali Marekani
Samidoh apata ajali Marekani
Image: Instagram

Wiki chache zilizopita, afisa wa polisi ambaye pia ni mwanamuziki wa miziki ya Kikuyu, Mugithi, Samidoh alisafiri nchini Marekani kwa ziara ya kimuziki itakayochukua zaidi ya mwezi mmoja.

Kwa wiki kadhaa sasa, msanii huyo amekuwa akifanya matamasha katika kumbi mbalimbali za starehe majimbo tofuati Marekani, na hata wiki jana alisherehekea siku yake ya kuzaliwa akiwa nchini humo.

Juzi ametangaza kwamba alipata ajali iliyomsababisha kukimbizwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji dharura ya haraka ambapo ilimbidi kuahirisha ziara yake.

Kupitia kurasa zake mitandaoni, Samidoh aliwaomba radhi mashabiki wake waliokuwa wanasubiria kutumbuiziwa naye katika eneo la Spokane.

Alisema kwamba alipata ajali na hivyo kuzuiliwa kusafiri huku akisema ameahirisha ziara hiyo mpaka wakati mwingine tena.

“Familia yangu ya Spokane mugithi, inasikitisha kuwa onyesho la leo lililazimika kuahirishwa Ajali mbaya ilitokea asubuhi ya leo na kunipeleka kwa E.R , hivyo kutoweza kusafiri kwa onyesho la leo. Tafadhali vumiliana nasi kwa usumbufu wowote uliojitokeza. Onyesho litapangwa upya hadi tarehe ya baadaye,” Samidoh alisema.

Japo alisema kila kitu kiko sawa, mamia ya mashabiki wake bado wana wasiwasi wa kutaka kujua kwa ufupi ni ajali gani hiyo ilimtokea mpaka kumfanya kukimbizwa katika chumba cha dharura.

Siku mbili zilizopita na akiwa bado kwenye ziara, Samidoh alisherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa mtindo huku akishangazwa na keki jukwaani. Mwimbaji wa Mugithi alipigwa na butwaa kwani hakutarajia mashabiki wake wangekuwa na mawazo kiasi cha kumnunulia keki ya kifahari.

Msanii huyo alishindwa kuacha kutabasamu huku akikabidhiwa keki jukwaani na mmoja wa mashabiki wake.