Wikendi iliyopita ilikuwa moja yenye majonzi na ukungu mkubwa katika taifa la Tanzania kufuatia ajali ya ndege ya kampuni ya Precision Air iliyoanguka ziwa Victoria.
Katika ajali ile, kijana mmoja mvuvi alionekana kuwa mstari wa mbele na mashua yake kuendesha shughuli ya uokoaji ambapo vyanzo vya habari vilikusanya habari kuwa alifanikisha uokoaji wa watu zaidi ya 24 kutoka kwa ndege hiyo.
Vyombo vya habari vilimtambua kwa jina Jackson Majaliwa ambaye ni mvuvi kutoka Bukoba ambapo ndege hiyo ilitarajiwa kutua kabla ya kuyumbishwa na kujipata ziwani.
Taarifa za hivi punde zinaripoti kuwa rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kijana huyo kupewa ajira katika jeshi la zimamoto na uokoaji mara moja kwa kitendo chake cha uzalendo na ujasiri wa kuokoa maisha ya makumi ya wahanga wa ajali ya ndege ya Precision Air.
Hilo limesemwa leo Jumatatu, Novemba 7, 2022 na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim “Majaliwa wakati wa ibada maalum ya kitaifa ya kutoa heshima za mwisho kwa miili 19 waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea jana Jumapili. Majaliwa amesema pamoja na mambo mengine, kijana huyo atapewa mafunzo zaidi ya uokoaji na kujengewa ujasiri wa kushiriki shughuli mbalimbali za uokoaji,” jarida la Mwananchi liliripoti.
Kijana Majaliwa Jackson tayari amekabidhiwa zawadi ya Shilingi milioni moja pesa za kitanzania kama ishara ya kutambua juhudi na moyo wake wa kujitolea zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila.