Mwakilishi wadi wa Kileleshwa Robert Alai amesema bintiye kiongozi wa Azimio Raila Odinga Winnie Odinga anafaa kuwa na wadhifa wa EALA, si kwa sababu yeye ni bintiye Raila bali kama mtu binafsi.
Winnie ni miongoni mwa wateule sita ambao waliteuliwa na ODM kwa Bunge la Afrika Mashariki.
Katika taarifa yake Ijumaa, Alai alisema Winnie hafai kuadhibiwa kwa sababu anatoka katika ukoo wa Raila.
"Acha Winnie Odinga awe mbunge wa EALA. Alizaliwa mwanasiasa na ni wito wake. EALA ni mwanzo mzuri kwake," alisema.
"Familia ya Odinga ni ya kipekee ya kisiasa. Wamefanya mema zaidi kwa Kenya. Mwache Winnie."
Wengine walioteuliwa na ODM ni pamoja na mfanyabiashara Suleiman Shahbal, Mohamed Diriye, Timothy Bosire, Beatrice Askul, na Justus Kizito.
Sita hao wanawakilisha kaunti za Mombasa, Wajir, Nairobi, Nyamira, Turkana na Kakamega.