Baada ya mbunge wa Fafi, Salah Yakub kuzua tafrani nchini kwa matamshi yake kuwa atawasilisha mswada bungeni wa kufanyia kipengele cha katiba marekebisho ili kuondoa mihula ya urais, kiongozi wa chama cha Roots msomi George Wajackoyah amejibu vikali madai hayo.
Wakili huyo msomi ambaye alimaliza namba 3 katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka 2022 alimzomea rais Ruto na kumtaka afanye udhubutu wa kuondoa kipengele hicho cha katiba kama kweli yeye ni mwanaume.
Wajackoyah alimwambia rais Ruto kuwa hata yeye anafaa kujua amekalia kiti cha urais na kushikilia dola kama mkuu wa majeshi kwa muda tu wala wakenya hawawezi mruhusu kubaki madarakani milele kama ambavyo mbunge huyo wa Fafi alidokeza.
“Kwako Ruto huu ndio ujumbe kwako, wewe ni rais na umekalia hicho kiti cha urais kwa muda tu, usijaribu kuleta upuuzi wako eti unataka kukalia hicho kiti milele. Unajaribu kutuma wabunge na watu kama Farouk eti mnataka kutafuta mbadala kuona vile hii serikali itakuwa ya kurithishwa. Mimi ninaambia Ruto jaribu. Eti mtoe katiba, ndio ukae huku milele..” Wajackoyah alizungumza kwa hasira.
Alimwambia kuwa akalie hicho kiti akijua kuwa hata rais Uhuru Kenyatta naye alikikalia na sasa ameondoka na kukiacha vile vile.
“Wewe kalia hicho kiti ukijua hata rais Uhuru Kenyatta pia amekuwa hapo na sasa angalia mahali alipo. Mimi ndio kiongozi wa upinzani rasmi na tunahitaji watu wachanga katika nyadhifa za uongozi wan chi hii,” Wakili huyo msomi alitema moto.