Mkenya asifiwa kwa kurudisha Ksh 91K alizotumiwa kimakosa

Mkenya huyo anayeishi Marekani alikuwa amelala na kuamka ambapo alipata ametumiwa pesa.

Muhtasari

• Mwanaume huyo alisema kuwa aliamua kurudisha pesa hizo si kwa sababu anazo nyingi bali kutokana na mafunzo ya uadilifu aliyopewa na wazazi wake.

Image: Keziah//Facebook

Ukimpata mtu akikuambia kwamba nchini Kenya au hata duniani hamna watu wazuri waliobaki basi huyo atakuwa anakuongopea.

Mwanaume mmoja Mkenya amepokea sifa sufufu kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuelezea jinsi alivyorudisha pesa takribani laki moja  kwa mtu ambaye alimtumia pesa hizo kimakosa.

Mwanume huyo kwa jina Kiziah alipakia msururu wa picha za maongezi yao kwenye mtandao wa Facebook mpaka pia akionesha jinsi alifanikisha mchakato wa kurudisha pesa hizo  baada ya yule aliyetuma kimakosa kumwandikia ujumbe wa barua pepe akimuomba kumrudishia pesa hizo kwani alikosea namba moja na zikaingia kwake.

Kulingana na Kiziah, alirudisha pesa hizo si kwa sababu alikuwa na hela nyingi bali kutokana na mafunzo aliyofunzwa na wazazi wake kuwa mkweli.

“Mkenya mwenye bidii alinitumia kimakosa 100,000/- nikiwa nimelala. Niliamka na kupata ombi lake la barua pepe. NIKAMRUDISHIA, Sio kwa sababu nina pesa BALI Kwa sababu ndivyo nilivyofunzwa na wazazi wangu. Sabato njema,” mwanaume huyo aliyetajwa kuwa mwenye roho nzuri kutokana na kitendo hicho aliandika Facebook.

Alipakia picha za mazungumzo yote jinsi jamaa huyo kwa jina James alimwandikia barua pepe akimbembeleza kumrudishia pesa hizo.

“Naomba kurudishwa kwa KSh 91,988 nilizotuma kimakosa kwenye akaunti yako kupitia paybill mnamo Novemba 11, 2022 saa 2:34 mchana. Angalia maelezo kwenye barua pepe," barua pepe kutoka kwa James kwa Kiziah ilisoma.