Mshukiwa wa ujambazi auawa huku polisi wakiimarisha doria kukabili utovu wa usalama

Imebainika kuwa siku za wahalifu wa Nairobi zimehesabiwa kwani polisi wamechangamka

Muhtasari

• Polisi walipata panga mbili, bunduki ya kujitengenezea nyumbani na simu ambazo zinaaminika kuibwa kwa wananchi.

Pingu
Image: Radio Jambo

Mshukiwa wa ujambazi aliyekuwa amejihami aliuawa kwa kupigwa risasi mjini Thika na polisi usikuwa kuamkia leo huku idara ya polisi ikiimarisha doria kudhibiti hali ya usalama nchini.  

Kulingana na maelezo ya idara ya DCI jambazi huyo alikuwa miongoni mwa genge la washukiwa watatu ambao wamekuwa washambulia watu kwenye barabara ya Cascade Premier.

Mshukiwa alipigwa risasi alipokuwa akijaribu kutoroka maafisa wa polisi.

 "Tukio hilo liliwafanya majambazi wengine ambao walikuwa wamejihami kwa panga na bunduki kutoroka . Polisi walifanikiwa kumtia mbaroni mshukiwa mmoja huku mwenzake akitoroka ," DCI walisema.

Polisi walipata panga mbili, bunduki ya kujitengenezea nyumbani na simu ambazo zinaaminika kuibwa kwa wananchi.

Pikipiki isiyo na nambari ya usajili iliyokuwa ikitumiwa na majambazi hao pia ilinaswa na maafisa.