Msanii afariki aki'shoot video baada ya boti yake kupinduka majini

Tanzia hiyo ilifichuliwa na msanii mwenza kutoka Malawi ambaye alikuwa wakati wa tukio hilo.

Muhtasari

• Msanii huyo alikuwa anajulikana maarufu kama Diamond, huku wengi wakimfananisha katika vitu vingi na msanii Diamond Platnumz wa Tanzania.

Msanii wa Zambia aliyefariki maji
Msanii wa Zambia aliyefariki maji
Image: Hisani

Msanii maarufu mjini nchini Zambia kwa jina Mozy B ameripotiwa kufariki dunia wakati alikuwa katika harakati za ku’shoot video ya ngoma yake mpya.

Vyanzo vya habari kutoka nchini humo vilisema kuwa msanii huyo mkaazi wa mji wa Lundazi alifariki baada ya boti alilokuwa akitumia ku’shoot video majini kupinduka na kumzamisha majini.

Msanii huyo alikuwa anajulikana maarufu kama Diamond, huku wengi wakimfananisha katika vitu vingi na msanii Diamond Platnumz wa Tanzania. Habari hizo zilitaarifu kuwa ndani ya boti hiyo kulikuwa na watu watano lakini wengine wanne walifanikiwa kuogelea na ni Mozy B pekee aliyeshindwa kuogelea na kusababisha kifo chake.

Kufuatia tukio hilo baadhi ya watu walikimbilia eneo la tukio ambapo walifanikiwa kuuchukua mwili wa msanii huyo maarufu wa muziki wa Tumbuka na kuupeleka katika kituo cha afya cha Kasenga kwa matibabu lakini baada ya kufikishwa kituoni hapo alikutwa na umauti.

Kwa mujibu wa Amoeba msanii wa Malawi na rafiki yake aliyekuwepo wakati wa tukio hilo la kusikitisha ameiambia Chikaya news kuwa Mozy B amefariki dunia baada ya kushindwa kuogelea mara moja boti waliyokuwa wamepanda kupinduka.

"Ninatangaza kwa masikitiko makubwa kwamba rafiki yangu na kaka yangu Mozy B amekufa kufuatia kuzama kwa boti aliyokuwamo wakati wa kushoot video," alisema jamaa huyo mwenye huzuni.

Boti hiyo ilipinduka mwendo wa saa 12:00 mchana ya Jumapili tarehe 13 Novemba, 2022 na ilitangazwa kuwa amefariki baada ya msanii mwenzake na rafiki yake Amoeba kumkimbiza katika kituo cha afya.