Nilikunywa maji yaliyokuwa na maiti kwa siku mbili! Mwanamke asimulia

Alisema aligusa kitu laini kwenye maji ambayo ni ya kina kifupi mtoni mahali alikuwa akichota maji ya matumizi yake.

Muhtasari

• "Kwa siku mbili nilikuwa nimekita hema kwenye shamba letu ambalo liko karibu na mto. Nilikuwa napika, naoga  na kuchemsha maji ya mto huo ili ninywe," 4Low KE alisema.

• Mwanamke huyo alisema kuwa marehemu alikuwa mwanamume na huenda alianguka mtoni akivuka daraja akiwa mlevi.

Mfu akitolewa majini
Image: 4Low KE Twitter

Mama mmoja amesema kwamba alikunywa maji ya mto ambayo yalikuwa na maiti mfu kwa siku mbili bila kujua.

Kwenye twitter, mwanamke huyo alisema kuwa alikuwa amenunua hema ambayo alitaka kujaribu kupiga kambi nayo kisha akaamua kutumia karibu na nyumbani.

Alieleza kuwa aliamua kutumia hema hiyo kwenye shamba lao kwanza kabla ya kuitumia mahali pengine mbali na nyumbani.

"Kwa siku mbili nilikuwa nimekita hema kwenye shamba letu ambalo liko karibu na mto. Nilikuwa napika, naoga  na kuchemsha maji ya mto huo ili ninywe," 4Low KE alisema.

Alisema kuwa upande mwengine wa mto huo ni shamba la jirani yao ambalo limepandwa miwa.

Usiku, wakati mwezi unang'aa binti huyo alieleza kuwa alipenda kutembelea shamba hilo ili kuchuna miwa.

"Sasa siku ya pili nilipokuwa nikirudi shambani mwetu nikitoka kwenye shamba la miwa, niligusa kitu laini kwenye maji ambayo ni ya kina kifupi kwenye upande huo wa mto," alisema.

Alifafanua kuwa wakati huo hakushughulika kutaka kujua alichogusa kwa sababu hangeona vizuri kwenye giza.

Hata hivyo, bado alitaka kujua ni nini haswa alichogusa. Basi kulipokucha mwanamke huyo alielekea kwa mto.

"Upande huu wa mto huwa na kina kifupi. Nilifika hapo na alas! Ilikuwa maiti! ilikuwa mita chache na pale ambapo nilikuwa ninachota maji yangu!" alisema.

Alisema kuwa baada ya kuona hayo alichukua hatua ya kuwapigia polisi kisha mwili huo ukatolewa majini.

Mwanamke huyo alisema kuwa marehemu alikuwa mwanamume na huenda alianguka mtoni akivuka daraja akiwa mlevi.

"Alianguka kutoka kwenye daraja alipokuwa mlevi na ilikuwa wazi kuwa alikuwa hapo kwa siku kadhaa kwani samaki walikuwa wameanza kula vidole vyake vya mguu, kwa siku mbili nimekuwa nikinywa na kuoga maji yaliyokuwa na mfu! Nilihisi kukereka! alisema.