Kila chifu atapatiwa maafisa 5 wa polisi kuanzia Januari - Waziri Kindiki

Waziri huyo alikuwa anazungumza baada ya kumtembelea chifu mmoja eneo la Mtwapa, kaunti y a Kilifi.

Muhtasari

• Tunataka kuhakikisha machifu wanawezeshwa kutekeleza sheria na kueleza sera za serikali. - Kindiki.

Waziri Kindiki akiwa na chifu wa Mtwapa
Waziri Kindiki akiwa na chifu wa Mtwapa
Image: Facebook//KindikiKithure

Waziri wa usalama wa ndani Kithure Kindiki ametangaza mwelekeo mpya unaonuiwa kudumisha Amani na usalama si tu mijini bali hata vijijini.

Akitoa muongozo huo, waziri Kindiki alisema kuwa serikali ina mpango wa kuwapa ulinzi machifu wote kote nchini wapatao elfu sita.

Alisema kuwa serikali inapanga kuwapa machifu hao kila mmoja ulinzi wa maafisa wa polisi watano ambao watakuwa wanaandamana nao katika kata zao kama njia moja ya kuimarisha usalama humu nchini. Hilo litatafsiriwa kwa angalau maafisa 30,000 walio chini ya machifu kote nchini.

Akizungumza katika afisi ya chifu wa Mtwapa mjini Kilifi alipofanya ziara ya ghafla, Waziri wa Usalama wa Ndani Kindiki Kithure alisema hatua hizo mpya zitatekelezwa kuanzia Januari mwaka ujao.

“Kila chifu atakuwa na angalau maafisa watano wa polisi waliounganishwa nao. Tunataka kuhakikisha machifu wanawezeshwa kutekeleza sheria na kueleza sera za serikali. Pia tunakabiliana na changamoto za kiusalama … lakini maafisa watano wa polisi kwa kila chifu wanapaswa kutumwa, kulingana na marekebisho ambayo tunataka kufanya ili kuhakikisha polisi pia wanatumwa kwa masuala muhimu ya usalama wa taifa,” Kindiki alisema.

Pia aliwaonya dhidi ya kujihusisha na siasa badala yake watumie ofisi zao kuwasilisha mambo chanya kuhusu serikali na sera na mipango yake huku wakihamasisha umma juu yao.

Aliwahakikishia machifu, wasaidizi wao na wasimamizi wengine wa serikali ya kitaifa katika mashinani msaada wa serikali, akiongeza kuwa mazingira yao ya kazi yataboreshwa ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi.

Alisema ni muhimu kuimarisha maafisa wa utawala wa serikali ya kitaifa ili kuimarisha usalama na ukusanyaji wa taarifa.