Nairobi: Wanafunzi waliovalia sare kusafirishwa bure bila kulipa nauli - Gov. Sakaja

Kiongozi huyo wa kaunti alisema haya baada ya kumalizika kwa mkutano baina yake na wahudumu wa matatu jijini.

Muhtasari

• Sakaja alisema kuwa mwanafunzi yeyote ambaye atakuwa amevalia sare yake rasmi ya shule yake atasafirishwa bila kuitishwa nauli.

Gavana Sakaja atangaza wanafunzi Nairobi kusafirishwa bure
Gavana Sakaja atangaza wanafunzi Nairobi kusafirishwa bure
Image: Facebook//Sakaja

Gavana wa Nairobi mheshimiwa Johnson Sakaja ametangaza kuwa ameafikiana na wahudumu wa sekta ya matatu za uchukuzi wa umma jijini Nairobi kuwasafirisha bila malipo wanafunzi wote wa shule katika kaunti hiyo.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao na wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma katika ukumbi wa City Hall, Sakaja alisema kuwa mwanafunzi yeyote ambaye atakuwa amevalia sare yake rasmi ya shule yake atasafirishwa bila kuitishwa nauli hata senti moja.

Kandio na hayo, vyanzo vya habari viliarifu kuwa gavana Sakaja alisema ataanzisha mazungumzo na maafisa wa trafiki ili kutafuta njia mbadala za kutokamata magari yatakayopatikana yamebeba wanafunzi kupita kiasi.

Haya yanakuja huku zikiwa zimesalia siku chache tu kwa shule za msingi na upili humu nchini zikitarajiwa kufungwa rasmi kupisha mitihani ya kitaifa na sherehe za siku kuu ya Krismas na mwaka mpya pia.

Kulingana na ratiba ya masomo, shule zinatarajiwa kuanza kufungwa wiki kesho na maandalizi ya mitihani ya kitaifa kuanza mwishoni mwa mwezi Novemba.

KICD walitoa ratiba ya masomo mwaka kesho na kudokeza kuwa masomo yatarejelea hali ya kawaida ambapo muhula wa kwanza utakuwa unaanza mwezi Janauri kwa mara ya kwanza tangu kusambaratishwa na janga la Korona miaka miwili iliyopita.