Bintiye Ruto atembelea 'Hustler' mmoja Nairobi, aburudika na glasi ya juisi yake

Charlene Ruto alionekana ameketi na glasi mkononi akibugia huku akisikiliza kwa makini hadithi ya mwanadada huyo mfanyibiashara wa chini.

Muhtasari

• Akiwa na zana kama vile Hustler Fund, atapanua biashara yake na kukuza mapato yake. - Charlene alisema.

Charlene Ruto akiwa katika duka la biashara ya mwanadada mmoja Kariobangi
Charlene Ruto akiwa katika duka la biashara ya mwanadada mmoja Kariobangi
Image: Twitter

Binti wa kwanza wa taifa, Charlene Ruto amepakia picha akionyesha jinsi alifanya ziara ya kushtukiza katika biashara ya mwanadada mmoja kwenye mtaa mmoja wa mabanda jijini Nairobi na hata kuburudisha na vyakula vyake.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, binti wa rais Ruto alisema alimtembelea mwanadada huyo wa kufanya biashara za kuuza sharubati na milkshake katika mtaa wa Kariobangi viungani mwa jiji la Nairobi.

Charlene alisema kuwa alimsikiliza mwanadada huyo kwa makini jinsi alivyosimulia kuwekeza vipesa vyake vichache mpaka kuanzisha biashara yake ya kupambania maisha.

Kando na kumsikiliza, binti wa rais alionekana akijivinjari kwa glasi ya juisi ya mwanadada huyo huku akiuliza watu kama wako tayari kupokea mkopo wa Hustler Fund kutoka kwa serikali ya babake – mkopo ambao maudhui yake ni kuwasaidia wapambanaji wa chini kuanzisha biashara ndogo ndogo za kujikimu kimaisha.

“Nilimtembelea kijana mmoja katika duka la Kariobangi Kusini leo na kusikiliza hadithi yake kuhusu jinsi alivyohifadhi pesa za kutosha kuanzisha duka lake la juisi na maziwa. Akiwa na zana kama vile Hustler Fund, atapanua biashara yake na kukuza mapato yake. Je, uko tayari kwa mkopo wa The Hustler Fund?” Charlene Ruto aliuliza.

Baadhi ya watu kwenye mtandao huo walizua madai kuwa ndio ameanza safari ya kutembea kote nchini kutafuta wateja wa kupewa mikopo ya Hustler ili kujikimu kimaisha.