"Mnaopinga sera yetu ya GMO mtaungua jehanamu!" - Kuria amjibu Raila na timu yake

Akizungumza na vyombo vya habari kutoka afisi zake Upperhill Nairobi, Odinga alimtaka Kuria kusitisha hatua ya kuagiza mahindi ya GMO gunia 10M

Muhtasari

• Kulingana na bwana Raila, suala la GMO si jambo la kukurupukiwa tu hivi bali linahitaji majadiliano ya kina na pia kuhusishwa kwa umma.

Kuria asema umaarufu wake katika ngome ya Raila uko juu
Kuria asema umaarufu wake katika ngome ya Raila uko juu
Image: Maktaba

Waziri wa Viwanja, biashara na uwekezaji, Moses Kuria ameendelea kutetea hatua yake ya kusema kwamba ataruhusu uagizwaji wa gunia milioni 10 za mahindi ya GMO kuja humu nchini ili kuwasitiri Wakenya wanaokufa njaa.

Baada ya matamshi yake hivi majuzi kuwa Wakenya huwa wanakufa kila mara na kuna vitu vingi vinavyohatarisha maisha na kwamba kuongeza mahindi ya GMO katika orodha hiyo si tatizo, sehemu ya Wakenya haswa viongozi kutoka mrengo wa upinzani wamekuwa wakipinga kauli hiyo na hata kumtaka Kuria kuomba wakenya msamaha kwa matamshi kama hayo.

Jumapili mchana kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga alimtaka Kuria kuomba radhi na pia kusitisha hatua hiyo ya kuruhusu mahindi ya GMO kuja humu nchini kama njia ya kupiga njaa vita.

Kulingana na bwana Raila, suala la GMO si jambo la kukurupukiwa tu hivi bali linahitaji majadiliano ya kina na pia kuhusishwa kwa umma kwa sababu hatari za GMO kiafya ni nyingi na zinafaa kujadiliwa hadharani.

Kuria amejibu vikali huku akisema kwamba wale wote wanaopinga kuagizwa kwa mahindi ya GMO watafia jehanamu kwani wengi wao wana vyakula vya kuwasitiri na wanapinga GMO ambayo yanafaa kuja kama suluhisho kwa makali ya njaa inayowakumba mamilioni ya Wakenya katika sehemu mbalimbali.

“Haifai kabisa kwa wavivu matajiri nwa kuTwitterati huku wakiwa na bakuli la pizza na vijisamaki kuendelea kushambulia sera yetu ya GMO huku Hustlers wakifa kwa njaa na nyama ya punda yenye sumu. Mtaungua kuzimu,” Kuria alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.