Wakenya waibua video Raila Odinga akisukuma serikali kukubali GMO 2011 (video)

Odinga kwa sasa amekuwa mstari wa mbele akipinga vikali hatua ya serikali kuruhusu uagizwaji wa mahindi ya GMO kuja humu nchini.

Muhtasari

• Katika video hiyo, Odinga anasikika akiirai bunge kuwa hata mataifa yenye ustawi mkubwa kisayansi yamekubali GMO na hivyo haikuwa hatari kwa afya.

• Kwa sasa bwana Odinga yupo mstari wa mbele kupinga hatua ya serikali kuagiza gunia milioni 10 za mahindi ya GMO.

Ni zaidi ya mwezi mmoja sasa tangu suala la mahindi ya GMO kuletwa humu nchini lianze kuzua mjadala mkali mitandaoni, huku serikali ya rais William Ruto ikisema ipo tayari kukubali mahindi hayo kuagizwa kuja humu nchini ili kuwanusuru wakenya wanaoteseka kwa njaa.

Kwa upande mwingine, muungano wa upinzani ukiongozwa na kiongozi mkongwe Raila Odinga umekuwa msrari wa mbele ukipinga uagizwaji wa mahindi hayo katika kile ambacho wanasema GMO inahatarisha afya ya wakenya na kuwa madhara yake ni sharti kwanza yajadiliwe bayana kabla ya kufanya uamuzi wa kuaiza mahindi hayo.

Wiki jana, waziri wa viwanja, biashara na uwekezaji Moses Kuria aliibua madai kuwa alikuwa anatia notisi kwenye gazeti la serikali kuruhusu uagizwaji wa mahindi ya GMO yapatao hunia milioni kumi bila tozo yoyote kwa miezi sita ijayo.

Kuria alitetea hatua hiyo kwa kusema kwamba ni sharti wakenya wanaokufa njaa watafutiwe njia ya kuwasaidia na mbadala yake ni mahindi hayo ya GMO ambayo yatapunguza gharama ya bei za unga wa mahindi madukani na pia kurahisisha maisha.

 Odinga kwa mara nyingine alipinga hatua hiyo na kumtaka Kuria na rais Ruto kubatilisha hatua hiyo kwani uagizwaji wa mahindi ya GMO ni kuhatarisha afya ya Wakenya, akisema kuwa mahindi hayo si salama kabisa.

Lakini Wakenya wiki hii wameingia kwenye makabrasha ya zamani na kuibua video ya zamani miaka 11 iliyopita ikimuonesha Odinga akiisukuma serikali ya hayati rais Kibaki kukubali uagizwaji wa mahindi ya GMO.

Katika video hiyo ambayo sasa imezua mjadala mpya haswa ikizingatiwa wakati huu ako upande mwingine wa kupinga mahindi ya GMO, wakati huo Odinga alikuwa akiwasilisha hoja zake bungeni akiwa kama waziri mkuu na kusema kwamba sheria ya bunge ilifaa kupitishwa bila kusita ili kuruhusu mahindi hiyo uja Kenya kuokoa wale waliokuwa wanashambuliwa na njaa kali kipindi hicho.

“Tukumbatie sayansi, na tunafaa kujua kwamba bwana spika sayansi inazidi kusonga mbele. Uhafidhina utaua uvumbuzi bwana spika. Mataifa ambayo nimetaja hapa ni yale ambayo yamekumbatia sayansi na yamebobea na hayawezi kukubali wananchi wake kutumia vyakula vya GMO kama ni hatari kwa afya,” Odinga alisema katika klipu hiyo.