Miguna aondoka nchini, mwezi mmoja baada ya kurejea

Wakili huyo alirejea nchini mnamo Oktoba 20 baada ya kufungiwa kutotua Kenya kwa zaidi ya miaka 4 tangu mwaka 2018.

Muhtasari

• Miguna alisema kuwa atatoa mwelekeo sahihi kwa watu wa Nyanza ikiwemo kumng'atua Odinga kama msemaji wa eneo hilo.

Miguna akiwa katika uwanja wa ndege tayari kuondoka nchini
Miguna akiwa katika uwanja wa ndege tayari kuondoka nchini
Image: Facebook

Wakili Miguna Miguna ameondoka nchini kuelekea nchini Uingereza, wiki kadhaa baada ya kurudi nchini kutoka uhamishoni.

Akidhibitisha taarifa hizi, Miguna japo hakusema kile kinachomsababisha kuondoka nchini, aliweka wazi kwamba hivi karibuni atarejea na kuendelea na mishe zake za kumpiku kiongozi wa ODM Raila Odinga kama msemaji wa eneo la Nyanza.

“Naelekea London, na mpenzi, nitarejea hivi karibuni, viva!” Miguna Miguna aliandika mitandaoni.

Miguna alirejea nchini mnamo Oktoba 20 wakati taifa lilikuwa linasherehekea siku ya mashujaa na hata kuhudhuria sherehe hizo katika uwanja wa Uhuru Gardens jijini Nairobi zilizoongozwa na rais William Ruto.

Kurejea kwake kulifikisha kikomo uhamisho wake wa kulazimishwa uliodumu kwa zaidi ya miaka 4 nchini Canada baada ya kutofautiana kisiasa na aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta na kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga.

Kurejea kwake nchini kulikuwa kumewekewa vizuizi vingi vilivyonyima mashirika yote ya ndege kibali cha kuweza kumsafirisha kuja nchini lakini alipata afueni baada ya Ruto kushinda urais na kumuondolewa vizuizi hivyo vyote.

Baada ya kutua nchini, Miguna hajakuwa mzungumzaji sana kama wengi walivyokuwa wamemzoea kweney mitandao ya kijamii bali aliahidi kuwa ataanzisha mchakato wa kuhakikisha anamvua Odinga mamlaka ya kuwa msemaji wa eneo la Nyanza katika kile alisema kwamba eneo hilo limekuwa likitengwa kimaendeleo kutokana na Odinga kuwa msemaji wake na kiongozi wa upinzani kwa kile serikali mpya kwa miaka mingi.