(+video) Mwanasiasa wa Nyandarua atokwa jasho kujieleza kwa lugha ya Kiingereza

Diwani huyo maalum alishindwa kujieleza katika lugha ya Kiingereza na hii si mara ya kwanza kuonekana aking'ang'ana kujieleza kwa lugha hiyo.

Muhtasari

• Mwanasiasa huyo alijipata pagumu wiki kadhaa zilizopita baada ya kushindwa kuisoma hotuba aliyokuwa ameandikiwa, hotuba ambayo ilikuwa yake ya kwanza bungeni.

Diwani mteule katika kaunti ya Nyandurua amegeuzwa kichekesho baada ya video yake akijitutumua bila mafanikio katika kujieleza kusambaa pakubwa mitandaoni.

Katika video hiyo, Milka Muthoni, ambaye alikuwa akitoa hotuba yake wakati wa mabishano ya kikao cha bunge cha kaunti akitoa maoni yake katika lugha ya Kiingereza, aling’ang’ana kujieleza lakini mwisho wa siku ikawa taabu juu ya mateso kwani wengi walisema kuwa hawakuwa wanaelewa mwakilishi huyo wa wadi mteule alikuwa anajaribu kuzungumza nini kwa ufasaha.

“Nasema ahsante sana bwana Spika kwa sababu unanilinda katika nchi nzima. Nasema ahsante sana. Haya, Naishukuru kamati ya biashara ya nyumba kwa kufanya kazi nzuri na pia naunga mkono uteuzi wa Emmah Kibiru kwa sababu anatoka katika kata yangu na wananchi wa kata ya Kinangop Kaskazini wamenyenyekea sana kwa sababu ya uteuzi wa Emmah. Ninamshukuru MCA wa eneo langu Wambugu King’ori kumpa Emmah Kibiru baraka. Nasema asante sana,” Mwanadada huyo alionekana aking’ang’ana kubananga lugha hiyo.

Bi Muthoni pia alipata wakati mgumu wiki kadhaa zilizopita alipokuwa akitoa hotuba yake ya kwanza katika bunge la kaunti hiyo. Ijapokuwa hotuba hiyo iliandikwa, Bi Muthoni alipata matatizo katika kutamka mbolea na ruzuku huku ukosefu wake wa uwiano ukitawala hotuba hiyo.

 Hii si mara ya kwanza wanasiasa wanajivunjia heshima kwa wananchi kwa kuonesha utepetevu wao katika kuzungumza Kiingereza kwani hata baadhi ya wabunge walijipata katika hali ngumu wakati wa kuapishwa katika kuhudumia bunge la 13 miezi miwili iliyopita.