Gavana Sakaja apuzilia mbali madai ya kuongezeka kwa bei ya ardhi Nairobi mwaka ujao

Sakaja alikuwa akijibu makala iliyochapishwa na chombo cha habari cha humu nchini siku ya Ijumaa

Muhtasari
  • Makala hayo yalikuwa yamegusia wamiliki wa majengo kuanzia Januari kulipa kiwango cha Ksh.2,560 kila mwaka kwa ardhi iliyo chini ya hekta 0.1
Gavana Sakaja atangaza wanafunzi Nairobi kusafirishwa bure
Gavana Sakaja atangaza wanafunzi Nairobi kusafirishwa bure
Image: Facebook//Sakaja

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja amejitokeza kukanusha ripoti kwamba viwango vya ardhi jijini vitaongezeka maradufu kuanzia mwaka ujao kufuatia uthamini mpya wa mali.

Sakaja alikuwa akijibu makala iliyochapishwa na chombo cha habari cha humu nchini siku ya Ijumaa, akibainisha kuwa viwango hivyo havitaongezeka maradufu bali vitaongezeka kidogo tu.

Kulingana na Gavana, uthamini wa mwisho ulifanyika zaidi ya miaka 40 iliyopita, hivyo basi haja ya kufanya mapitio ya orodha ya uthamini.

“Hakuna viwango vinavyoongezeka maradufu. Tunapitisha orodha mpya ya uthamini na viwango viko katika 0.115% ya thamani ya tovuti ambayo haijaimarishwa. (Thamani ya mwisho ilikuwa 1980) Hii ina maana kuna ongezeko kidogo tu kutoka kwa kile wakazi wamekuwa wakilipa. Acha kupotosha watu,” aliandika kwenye Twitter.

Makala hayo yalikuwa yamegusia wamiliki wa majengo kuanzia Januari kulipa kiwango cha Ksh.2,560 kila mwaka kwa ardhi iliyo chini ya hekta 0.1 na Ksh.3,200 kwa hiyo zaidi ya hekta 0.1 lakini chini ya hekta 0.2.