Kambua afurahia mimba ya 3, asema aliwahi ambiwa yeye ni tasa

Kambua amewapa moyo wanadada ambao wako kwenye hali hiyo

Muhtasari

• Kwenye Instagram, Kambua alikumbuka jinsi alivyompoteza mwanawe wa pili na hisia za huzuni wakati huo.

• Alieleza kuwa anaelewa yote ambayo yanakuja na kuwa kwenye hali hiyo kwani alivunjika moyo baada ya kumpoteza mwanawe.

Kambua
Image: Kambua Muziki Instagram

Mwimbaji wa nyimbo za Injili, Kambua amepakia ujumbe huku akisherehekea kuwa mjamzito kwa mara ya tatu.

Kwenye Instagram, Kambua alikumbuka jinsi alivyompoteza mwanawe wa pili na hisia za huzuni wakati huo.

Mwimbaji huyo alieleza jinsi miaka iliyopita alipata ripoti kutoka kwa daktari kuwa hawezi kupata watoto ila Mungu amemjalia na kumpa nafasi ya kuwa mama.

"Mungu alikaa nami kwenye giza, na taratibu akaanza kuniinua. Alinikumbusha pia kwamba miaka iliyopita nilipokea ripoti ya daktari iliyosema mimi ni tasa. Wakati ulimwengu ukinidhihaki alinikumbusha kwamba alikuwa anashughulikia wema wangu na utukufu wake," Kambua alisema.

Mama huyo aliwapa matumaini wanawake ambao wamekuwa kwenye hali kama yake, hali ya kutamani mtoto, ya kumpoteza mtoto na hata kutoweza kupata watoto kabisa na kusema kuwa Mungu atawapa amani wanayotamani sana.

Alieleza kuwa anaelewa yote ambayo yanakuja na kuwa kwenye hali hiyo kwani alivunjika moyo baada ya kumpoteza mwanawe.

"Zaidi ya mwaka mmoja uliopita nilimshikilia mwanangu niliyethamini mikononi mwangu huku mwili wake mdogo ukiwa baridi akikata kamba. Nilikuwa kwenye giza nene mno. Nilifahamu hisia ya huzuni, sikudhani itakuwa hivyo. Lakini Mungu," mwimbaji huyo alisema.

Kambua alieleza shukrani yake na furaha kwa kuweza kuwa mama kwa mara nyingine tena na kueleza jinsi Mungu alivyomtoa kwenye giza.

Alisema jinsi hakutarajia kuwa siku hizo zitakuwa na mwisho ila sasa Mungu amempa sababu ya kuwa na furaha na kuwahimiza wanawake wengine.

Mama huyo anayetarajia alizidi kumpa Mungu sifa zake na kuwaeleza watu kuwa chochote kinachowatatiza watafanikia kupata.

"Hivi sasa mwanamke mahali fulani amejua kwamba mwili wake hauna "uwezo" wa kutosha wa kubeba watoto. Au mtoto wake hatakamilisha siku za ujauzito wake. Mwanamke ametoka tu kuharibikiwa mimba ... labda kwa mara ya tano. Mwanamke mahali fulani amejifungua mtoto mkamilifu, aliyelala. Ah najua huo uchungu. Ninaujua. Lakini pia najua kuwa Mungu anaponya- anatupa nguvu na ujasiri wa kusonga mbele. Mungu anatutarajia mema. Akuponye, akubebe, na kukurejesha 🦋🖤," mama huyo alisema.