Mama wa taifa Rachel Ruto na mke wa naibu rais mama Dorcas Gachagua Jumatano walihudhuria ibada ya maombi katika kanisa moja mjini Thika kaunti ya Kiambu.
Wawili hao walionekana pamoja katika ibada hiyo ambayo mama Rachel Ruto alisema ilikuwa na maudhui ya kutambua maadui wako.
“Hii ni mara ya kwanza ya mikusanyiko kama hii nchini Kenya, inayoongozwa na Mwinjilisti Dag Heward-Mills. Hayo ndiyo yalikuwa mafundisho leo, nilipopamba na kushiriki katika Kampeni ya Kuponya Yesu na Kutambua Maadui Hatari (IDEC) 2022 katika Kanisa la Kimataifa la Christian Church, Thika,” mama Rachel Ruto aliandika Twitter.
Mama Rachel Ruto alisema kuwa alifurahia kujifunza kutoka kwa biblia kuwa kina baba ni watu wa maana sana katika maisha ya mwanadamu.
Alinukuu kitabu cha Malaki akisema kuwa sisi wote tulitoka kwa Adam ambaye alikuwa mwanadamu wa kwanza aliyeumbwa kutokana na mfano wa Mungu mwenyewe.
“Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, nisije nikaipiga nchi kwa amri ya maangamizo. - Malaki 4:6. Katika Adamu, Mungu alitupa baba wa kwanza. Na, sisi sote ni wazao wake – Wanadamu,” alisema.
Katika ibada hiyo, Rachel waliandamana na mama Dorcas Gachagua ambaye ni mchungaji pia aliyekubuhu katika kueneza neno la Mungu kwa zaidi ya miaka 11 sasa.