Ilinichukua miaka 10 kukubali mimi ni mwathirika wa HIV - Mwanadada asimulia

Unyanyapaa huu ulikaribia kunifanya nijiue lakini kwa maombi, Mungu alinijia - alisimulia.

Muhtasari

• Kuishi na UKIMWI haikuwa kawaida kwa watu ambao hawana. Walinitazama kama mtu asiye na nia ya kushirikiana nami - Gloria Nawanyaga.

• Mwanadada huyo alisema alizaliwa na virusi hivyo na unyanyapaa enzi akiwa shuleni ulikuwa mwingi mno dhidi yake.

Gloria Nawanyaga, mwathirika wa virusi vya UKIMWI
Gloria Nawanyaga, mwathirika wa virusi vya UKIMWI
Image: Instagram

Desemba mosi ni siku ya kutoa hamasisho kuhusu ugonjwa wa ukimwi duniani. Siku hii husherehekewa kote duniani kuwahimiza wale wanaoishi na virusi vya HIV, kutoa hamasisho jinsi ya kujikinga kutokana na maambukizi mapya na pia kutoa mafunzo kutowanyanyapaa waathirika.

Gloria Nawanyaga ni mwanadada ambaye alizaliwa na virusi vya ukimwi nchini Uganda na Desemba mosi alishiriki mazungumzo ya kina katika runinga moja cnhini huko kuelezea safari yake ya kuishi na virusi hivyo kwa zaidi ya miaka 20.

Nawanyaga alisema kuwa wanaume wengi humhukumu kutokana na hali yake ya kuwa mwathirika wakisema kuwa amefanya mapenzi na wanaume wengi na kudhani huenda mmoja wao ndiye alimuambukiza virusi hivyo.

“Bado tunao watu wanaoamini hadithi na imani potofu kuhusu kuishi na virusi vya UKIMWI. Wanaume wengine wangeniuliza ni watu wangapi ambao nimelala nao wakidhani nimepata virusi kutokana na kujamiiana,” Gloria alieleza.

Kando na hapo, suala la unyanyapaa bado ni sugu kwa wathirika wengi wa virusi vya ukimwi, na kwa Nawanyaga, hali haikuwa tofauti.

“Kuishi na UKIMWI haikuwa kawaida kwa watu ambao hawana. Walinitazama kama mtu asiye na nia ya kushirikiana nami. Unyanyapaa huu ulikaribia kunifanya nijiue lakini kwa maombi, Mungu alinijia.”

“Wakati nikiwa shule ya upili, nilijaribu sana kutomwambia mtu yeyote kuhusu hali yangu kwa sababu nilipomwambia matron wangu katika shule fulani, hakufanya siri. Hilo lilinifanya nihama kutoka shule hiyo kutokana na unyanyapaa,” mwanadada huyo alieleza.

Kutokana na unyanyapaa huu kutoka kwa watu waliokuwa wakishiriki kwa ukaribu naye kwa muda mrefu, Nawanyaga alisema kuwa ilimchukua zaidi ya miaka 10 kujikubali na hali yake ya kuwa mwathirika wa UKIMWI.

“Ilinichukua miaka 10 kukubaliana na hali yangu ya kuwa mwathirika. Mama yangu aliponiambia kwamba nilikuwa mwathirika, ilinigusa sana kwa sababu nilifikiri ulikuwa mwisho wa maisha yangu,” alisema.

Nchini Kenya, ripoti inasema kwa mwaka uliopita, maambukizi ya virusi vya UKIMWI yaliongezeka kwa 7.3% huku kaunti ya Nairobi ikiongoza kwa maambukizi mapya 3,828 ikifuatwa na Kisumu 3,118, Homa Bay 2,696 na Siaya ikiwa na 2,180.