Mwanaume akimbia uchi kwenda kambi ya jeshi la KDF Kilifi, apigwa risasi hadi kufa

Inaarifiwa mwanaume huyo, 25, alishauriwa na mganga kuingia kwenye kambi ya jeshi akiwa uchi ili kufanikisha azma ya kuiba silaha.

Muhtasari

• KDF walijaribu kumtia woga kwa kufyatua risasi hewani lakini alizidi kutia jitihada za kuingia kambini.

• Alifyatuliwa risasi shingoni na kuuawa papo hapo.

Kielelezo
Kielelezo
Image: Maktaba//Kielelezo

Kioja kilishuhiwa katika kaunti ya Kilifi kwenye kambi ya jeshi la KDF ya Mariakani baada ya mwanaume aliyekuwa akikimbia uchi kupigwa risasi na afisa wa KDF na kufariki papo hapo.

Kulingana na taarifa, mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 25 alisemekana kushauriwa na mganga wa kienyeji kukimbia uchi kwenda kambi hiyo ya jeshi.

Licha ya afisa wa KDF aliyekuwa amelinda lango la kambi ya jeshi ya Mariakani kupiga risasi hewani ili kumtia woga asiingie, mwanaume huyo kwa jina Juma Kitsao Kombe alikuwa amejitahidi kuingia kwa fujo ndipo afisa akamfyatulia risasi shingoni na kumuua.

Jarida la The Star liliripoti kuwa Kombe alitambuliwa na mama yake. Marehemu anasemekana kuwa miongoni mwa genge ambalo limekuwa likiwahangaisha wenyeji wanaopakana na kambi hiyo.

Aliambiwa kuwa akiwa hana nguo angeweza kumfanya mlinzi huyo alale na hivyo angeondokana na nyara yoyote ambayo angeiba kambini.

Polisi walisema wanachunguza kesi hiyo. Wapelelezi kutoka Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) waliotembelea eneo la tukio walipata katuni mbili zilizotumika ambazo zitafanyiwa uchunguzi wa kina.

Mwili wa marehemu ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali Kuu ya Pwani ukisubiri uchunguzi wa maiti.

Wakaazi wa kaunti ya Kilifi baadhi wanaamini sana katika masuala ya kishirikina, uganga na uchawi ambapo katika miaka ya nyuma visa vya watu wazee kuuawa na watoto wao kwa kushukiwa kuwa wachawi vimekuwa vikiripotiwa.