Sihitaji kuwamia urais wa mwaka 2027 lakini pia sijasema siwezi wania - Raila Odinga

Aliwataka waandishi wa habari kulielewa hilo kwa ufasaha na kusema kuwa huwa wanamnukuu vibaya mara nyingi.

Muhtasari

• Iwapo atawania katika uchaguzi huo, Odinga ataweka rekodi ya mtu aliyewania mara nyingi zaidi urais, kwani itakuwa mara ya 6.

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: Hisani

Kinara wa ODM na muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga amenyoosha maelezo kuhusu uwezekano wake kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2027.

Akizungumza na Citizen TV usiku wa Jumanne Desemba 27, Odinga aliwatuhumu waandishi wa habari kwa kumnukuu vibaya mara nyingi kuhusu azma yake ya kujaribu bahati kwa mara nyingine tena katika kuongoza taifa la Kenya.

Odinga alisema kuwa hana haja ya kuwania urais mwaka huo lakini pia akasema hajaweka wazi kuwa hatawania huku akiibua maswali mengi kuliko majibu vichwani mwa Wakenya.

“Nataka mlichukue hili kwa umakini mkubwa kwa sababu wanahabari wakati mwingine wananinukuu vibaya. Sihitaji kuwamia urais wa mwaka 2027 lakini pia sijasema siwezi wania,” Odinga alisema.

Suala la Odinga kuwania urais tena mwaka 2027 limekuwa likiwagawanya baadhi ya wafuasi wake ambao wanamtaka kumuunga mtu mwingine mkono huku wengine pia wakisema hakuna mtu mwingine atakayeleta ushindani wa kutosha kwa rais Ruto kuliko Odinga.

Odinga amejaribu bahati yake katika kuwania urais kwa mara tano, safari zote akiambulia patupu na iwapo atakuwa debeni mwaka 2027 basi itakuwa ni rekodi mpya ya kuwania kwa mara ya sita mtawalia.

Licha ya maneno mengi kusemwa kuhusu kushindwa kwake katyika uchaguzi wa Agosti mwaka huu ambao kila dalili zilikuwa zinampendelea yeye, Odinga amepuuza maneno ya aliyekuwa ajenti mkuu Saitabao Ole Kanchory kuwa baadhi ya watu katika Azimio walichangia kuanguka kwake.

Alimtetea rais mstaafu Uhuru Kenyatta dhidi ya mashambulio ya baadhi ya viongozi wa Azimio kuwa alichangia pakubwa kushindwa kwa Odinga na kusema kuwa Kenyatta alifanya kazi yake vizuri kumpigia kampeni ila kwa bahati mbaya tu wakashindwa.