Mvulana mwenye umri wa miaka 17 kwa jina Noble Uzuchi anaripotiwa kuzuiliwa na Polisi nchini Nigeria kwa kuwapa ujauzito wanawake zaidi ya 10.
Kulingana na chombo cha habari cha Nigeria, PUNCH, Kamandi wa Polisi wa Jimbo la Rivers nchini Nigeria alifichua na kuzima operesheni ya kiwanda cha watoto katika maeneo ya serikali ya mitaa ya Obio/Akpor na Ikwerre jimboni humo.
Washukiwa wanne wamekamatwa kuhusiana na operesheni hiyo haramu na wasichana kumi wajawazito wameokolewa.
Kulingana na polisi, Uzuchi na Chigozie Ogbonna mwenye umri wa miaka 29 waliajiriwa na kundi hili ambalo lilifungua kiwanda cha kuzalisha watoto kwa ajili ya kibiashara.
“Kiongozi wa harambee hiyo, Peace Alikoi mwenye umri wa miaka 40, basi angehifadhi watoto na kuwalipa akina mama kiasi cha N500,000 (KES 138,406). Baadhi ya watoto wachanga pia waliuzwa. Polisi pia wamemkamata Favour Bright mwenye umri wa miaka 30 kuhusiana na operesheni hiyo,” Punch waliripoti.
Polisi walidokezwa kuhusu operesheni hiyo na kuchukua hatua haraka kutokana na taarifa hiyo na kuvamia nyumba mbili za jamii ya Igwuruta na Omagwa ambako waathiriwa walikuwa wamehifadhiwa.
Wahasiriwa ambao wengi wao walikuwa wajawazito waliokolewa na kuwekwa chini ya ulinzi kwa uchunguzi zaidi. Polisi pia wamelipata gari aina ya Honda Pilot Jeep kutoka kwa kiongozi wa harambee hiyo.
"Waathiriwa wote walikiri kwamba walishawishiwa kwa mauzo haramu ya watoto kwa sababu ya hitaji la kukabiliana na baadhi ya changamoto za kifedha," Iringe-Koko, mratibu wa polisi aliiambia Punch.
Kesi hiyo imehamishiwa katika Idara ya Upelelezi wa Jinai ya Serikali na juhudi zinaimarishwa kuwasaka na kuwakamata wanunuzi wa watoto ambao tayari wameuzwa.
"Hatutapumzika hadi wale wote waliohusika katika kitendo hiki kiovu wafikishwe mahakamani na kuwajibishwa kwa matendo yao," Iringa-Koko aliongeza.