"Raila ni baba wa taifa, tunamheshimu kwa hadhi yake!" - DP Gachagua akiwa Homabay

Wengi hawakutarajia hili kwani DP Gachagua amekuwa akimshambulia Odinga kwa maneno makali tangu kuchukua hatamu za uongozi.

Muhtasari

• “Tuna tofauti za kisiasa tu. Baba anaheshimiwa katika serikali yetu. Magari yake na ulinzi wake umetunzwa vyema" - Gachagua.

DP azidi kumshambulia Odinga vikali
DP azidi kumshambulia Odinga vikali
Image: Facebook

Tangu naibu wa rais Rigathi Gachagua na rais William Ruto wachukue hatamu za uongozi wa Kenya kama viongozi wa awamu ya tano, naibu huyo amekuwa akimchimba mikwara na maneno kiongozi wa Azimio la Umoja one Kenya, Raila Odinga.

Wengi walitarajia kuona mwendelezo huo wa maneno yake makali dhidi ya Odinga wakati wa ziara ya rais Ruto katika mkoa wa Nyanza ambapo Gachagua aliandamana naye.

Lakini kwa mshangao wa wengi, Gachagua safari hii alionekana muungwana na badala ya kumtupia maneno Odinga, alibadilisha wimbo wake na kumpa maua yake mqazuri huku akimtaja kama baba wa taifa ambaye anafaa kupewa heshima.

Katika kile ambacho kimezua mjadala mkali kwenye mtandao wa Twitter, Gachagua alimsifia Odinga akisema kuwa kiongozi huyo wa upinzani ni mtu mzuri mwenye heshima huku akifichua kuwa maslahi yake yatashughulikiwa na serikali ya Kenya Kwanza.

“Tuna tofauti za kisiasa tu. Baba anaheshimiwa katika serikali yetu. Magari yake na ulinzi wake umetunzwa vyema. Ni kiongozi wa Kenya ambaye anafaa kuheshimiwa kutokana na hadhi yake. Nyinyi nyote ni wa serikali hii inayoongozwa na Rais William Ruto,” Gachagua alisema wakiwa katika kaunti ya Homabay ambayo ni ngome ya Odinga.

Tangu mwaka jana walipochukua hatamu, Gachagua ambaye wengi wamemtaja kama mtu mwenye hasira aliendeleza mfululizo wa kumtupia Odinga maneno huku akimtaka kukaa mbali na serikali ya Kenya Kwanza kwa kile alisema kuwa hawawezi kumkaribisha kama ambavyo rais mstaafu Uhuru Kenyatta alivyofanya.

Kwa wakati mmoja, Gachagua alikosolewa na gavana wa Siaya James Orengo aliyemtaka kumpa Odinga heshima zake na badala ya kusema sana kumhusu, ajishughulishe na kuwafanyia Wananchi wa Kenya kazi ambayo walichaguliwa kufanya.