Askari afariki akijaribu kuruka ukuta wa loji kumtoroka mwanamke baada ya kitendo

Askari huyo anasemekana kujaribu kutoroka mwanamke wake baada ya kukaa naye ndani ya chumba cha gesti kwa zaidi ya saa tatu.

Muhtasari

• Askari huyo alisemekana kuingia katika gesti na mwanamke majira ya saa sita usiku, na ilipofika saa tisa usiku, alijaribu kutoroka mwanamke wake kwa kuruka ukuta.

• Kwa bahati mbaya, alianguka na kudungwa na kitu chenye ncha kali kichwani kupelekea kufariki kwake.

crime scene
crime scene

Mkaguzi wa polisi katika mkoa wa Arusha, wilaya ya Arumeru nchini Tanzania kwa jina Stewart Kaino mwenye umri wa miaka 47 anaripotiwa kufa alipofanya jaribio la kuruka ukuta wa nyumba za wageni akijaribu kumtoroka mwanamke ambaye tayari walikuwa wameshiriki tendo la ndoa naye.

Kulingana na taarifa kutoka taifa hilo jirani, Kaino aliingia katika gesti hiyo mwendo was aa sita usiku wa manane akiandamana na mwanamke mmoja ambaye hakutambuliwa kwa jina.

Baada ya kula raha naye kwa saa kadhaa, Kaino alifanya jaribio la kumtoroka mchepuko huyo kwa kuruka ukuta wa gesti lakini akaanguka na kuchomwa kichwani hadi kufa na kitu kilichotajwa kuwa na ncha kali.

“Majira ya saa sita, aliingia na mwanamke mmoja na kuandikisha katika kitabu cha wageni na kupewa chumba na kisha kuingia na mwanamke huyo, akiwa ameshika begi dogo la mgongoni na redio ya mawasiliano aliyokuwa nayo mkononi. Majira ya saa tisa usiku alitoka ndani ya chumba hicho na kumuacha mwanamke huyo akiwa amelala. Alikwenda nyuma ya nyumba hiyo na kuruka geti akiwa na lengo la kumtoroka mwanamke huyo ndipo alipoanguka na kuchomwa na kitu chenye ncha kali kichwani,” shuhuda ambaye hakutaka jina lake kuwekwa wazi aliiambia TanzaniaWeb.

Taarifa zinadai kuwa baada ya mlinzi wa gesti hiyo kusikia kishindo, alifika kwa haraka na kumkuta afisa huyo yuko chini na alikuwa anavuja damu kwa kasi huku begi lake amelishikilia mkononi.

Polisi walipoitwa na kifika eneo la tukio, walipata afisa huyo mwenzao tayari amekata Kamba na walipopekua begi lake walikuta redio ya mawasiliano, chupa ya bia na simu mbili, moja ikishukiwa kuwa ya mwanamke huyo ambaye alikuwa anajaribu kutoroka.

Polisi waliondoa mwili wa marehemu katika eneo la tukio na taarifa zilisema tayari ulikuwa umesafirishwa kwenda kwao Bukoba kwa ajili ya maziko kulingana na tamaduni za kidini, huku uchunguzi ukianzishwa kubaini taswira nzima ya tukio hilo.