DP Gachagua: Msimamo wetu kwa polisi kuwasindikiza walevi nyumbani haujabadilika!

DP alisema mfumo wa kuwarudisha watu nyumbani unatumika nchini Marekani ambapo maafisa wa usalama huwapeleka watu walevi nyumbani.

Muhtasari

• DP pia alisema mishahara na marupurupu ya polisi itaangaliwa ili kuwaepusha kutokana na majaribu ya kupokezwa hongo.

DP Gachagua asisitiza kuwa polisi watawasindikiza walevi nyumbani
DP Gachagua asisitiza kuwa polisi watawasindikiza walevi nyumbani
Image: Facebook

Naibu wa rais Rigathi Gachagua amesisitiza msimamo wake kuwa kauli aliyoitoa wakati wa kamoeni kuhusu mageuzi katika idara ya polisi bado ungalipo na hivi karibuni mageuzi hayo yatafanyika kama ambavyo waliahidi kipindi cha kampeni.

Akizungumza katika kaunti ya Homabay wakati wa ziara ya rais Ruto ya kimaendeleo eneo pana la Nyanza, Gachagua alisisitiza kuwa polisi watashrutishwa kuwasindikiza walevi nyumbani pindi wanapowakuta usiku wakipiga kelele kutokana na ulevi.

DP Gachagua alirudia maneno yake na kusema kuwa haifai polisi kuwapeleka walevi hao katika kituo cha polisi au kuwatia mijeledi bali inafaa wanawaweka kwenye gari la polisi na kuwasindikiza kwa kipole hadi nyumbani kwao.

“Polisi wanapaswa kujua kuwa raia wote ni marafiki zao. Wapeleke watu walevi kwa wake zao ili wapumzike wala si seli,” DP Gachagua alisema.

Hii si mara ya kwanza Gachagua alizungumzia ishu ya polisi kuwapa walevi msaada wa kuwapeleka nyumbani kwa familia zao pindi wanapowakuta usiku wakiwa wamelewa chakari.

Kipindi cha kamepni za Kenya Kwanza, Gachagua aligusia suala la polisi na kusema kuwa pindi watakapochukua uongozi, mishahara yao ingeangaliwa na kuongezwa, kuboreshewa mazingira ya kazi ili kuwaepusha kutokana na kupokea hongo pamoja pia na kuwarai kujenga urafiki mzuri na wananchi walevi kwa kuwapeleka nyumbani wakiwa walevi.

Gachagua kipindi hicho alisema kuwa hilo linafanywa Marekani ambapo walevi wanasindikizwa hadi manyumbani kwao kwa magari ya polisi wa kupiga patroli usiku.

“Hatutatumia polisi kujinufaisha binafsi. Hakuna haja ya kuwakamata watu siku ya Ijumaa na kuwaachilia Jumatatu (bila malipo). Hayo ni matumizi mabaya ya utawala.”