Rais Ruto ameniomba radhi kwa niaba ya serikali iliyopita - Miguna Miguna

"Samahani kwa kile ambacho Serikali ilikufanyia. Samahani sana. Haikuwa haki. Naomba radhi," Itumbi alinukuu msamaha wa Ruto kwa Miguna.

Muhtasari

• Miguna alisema kuwa alikubali msamaha huo moja kwa moja kutoka kwa rais Ruto.

• Ruto alikamilisha ziara yake Nyanza iliyochukua siku mbili na Miguna ataikumbuka ziara hiyo kama moja iliyompelekea rais kumkuta na kumuomba radhi.

Hatimaye Ruto amuomba Miguna radhi
Hatimaye Ruto amuomba Miguna radhi
Image: Twitter

Wakili mbwatukaji Miguna Miguna amefichua kuwa hatimaye rais William Ruto alimuomba msamaha kutokana ma madhira ambayo serikali iliyopita ambapo alikwa kama naibu rais ilimfanyia kwa kumfukuza nchini kwenda Canada.

Miguna alisema kuwa ziara ya Ruto katika eneo la Nyanza haikukamilika tu kwa kuzindua miradi ya maendeleo bali pia alifanya haki kwa kumfuata moja kwa moja na kumuomba msamaha kwa kuhangaishwa na serikali yao iliyokuwa ikiongozwa na rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Wakili huyo kupitia Twitter alipakia picha wakiwa wamesalimiana na rais Ruto na kusema kuwa hatimaye alijihisi kufarijika baada ya kiongozi wa taifa kuwasilisha msamaha kwa niaba ya serikali iliyopita, mwenyewe pasi na kutuma mtu.

“Mheshimiwa William Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, mapema leo asubuhi AMENIOMBA RADHI kwa niaba yake na kwa niaba ya Serikali kwa unyama niliofanyiwa na utawala uliopita. Nakubali msamaha,” Miguna aliandika.

Japo hakusema kile ambacho rais Ruto alimwambia lakini maneno ya Ruto yalinukuliwa na mwandani wake wa karibu, Dennis Itumbi ambaye alisema kuwa rais alitamka msamaha wake kwa njia ya kipekee kwa Miguna.

"Samahani kwa kile ambacho Serikali ilikufanyia. Samahani sana. Haikuwa haki. Naomba radhi," Itumbi alimnukuu rais Ruto.

Aliyekuwa kamishna wa IEBC Roselyn Akombe ambaye pia alitoroka nchini mwaka 2017 na kurejea wiki chache zilizopita alimpongeza rais Ruto kwa kutoa msamaha wa kipekee kwa Miguna, huku akisema kuwa msamaha huo japo ulikuja kuchelewa lakini hatimaye haki imeonekana kutendeka, na kuwa hakuna mwanadamu anayestahili kupitia kile ambacho Miguna alipitia mikononi mwa polisi akillazimishwa kuondoka nchini.

“Msamaha wa muda muafaka lakini kubwa kwamba imetokea. Hakuna mwanadamu anayepaswa kupitishwa kwa kile daktari @MigunaMiguna alipitia,” Akombe alisema.

Miguna alirejea nchini mwaka jana mwezi Oktoba baada ya kuondolewa vizingiti vyote ambavyo serikali iliyopita ilikuwa imemuwekea tangu mwaka 2018 alipofanya jaribio la kumuapisha kinara wa NASA kipindi hicho, Raila Odinga, jambo ambalo liligeuka kuwa mwanzo wa picha mbaya maishani mwake baada ya Odinga kufanya maridhiano na rais Kenyatta.